Na John Stephen, MNH
Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza kutumia mitandao ya simu, kadi maalimu na
kadi za benki kwa ajili ya kulipia huduma za matibabu ili kuthibiti changamoto
za upotevu wa fedha na wizi katika ukusanyaji wa mapato ya hospitali hiyo.
Mpango wa kutumia njia za
kieletroniki umelenga kukusanya mapato zaidi ili kuiwezesha hospitali hiyo
kukabiliana na changamoto mbalimbali za uendeshaji na kutoa huduma bora
kwa wagonjwa.
Lengo la
hospitali hiyo ni kuongeza mapato na kupunguza matumizi na kutengeneza
mazingira ya kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wagonjwa mbalimbali
nchini.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na
Huduma kwa Wateja, Bwana Aminiel Aligaesha, hospitali hiyo imelenga pia
kuimarisha njia za ukusanyaji mapato ili kuboresha huduma za matibabu na
kuboresha maslahi kwa wafanyakazi.
“Hospitali
imelenga kuboresha wadi za kulaza wagonjwa wanaohitaji huduma na malazi
binafsi, kuhakikisha wagonjwa wanachangia huduma za matibabu na kuboresha mfumo
wa kuandaa hati za madai kwa kampuni na mifuko ya Taifa ya bima ya afya.
“Hospitali
imekusudia kutoa motisha na kuwahamasisha madaktari kuwaona wagonjwa kwa wingi
wanaolipia huduma ili kuwavutia kutibiwa katika hospitali hii,” imesema taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo
imeeleza kwamba hospitali hiyo imedhamiria pia kutoa motisha kwa wafanyakazi
wengine ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi.
Katika hatua nyingine,
hospitali hiyo imeweka mikakati ya kupunguza gharama za kununua dawa na vifaa
tiba kutoka viwandani (Manufacturers)moja kwa moja.
“Kwa mfano, baada ya kupata
kibali kutoka TFDA, Hospitali imenunua dawa za figo
(immunosuppressant) kutoka India kwa Sh 226 milioni wakati hapa
nchini zingegharimu Sh 500 milioni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, hospitali
hiyo imeagiza nyuzi za kushonea wagonjwa (sutures) kutoka
kiwandani (Ethicon)kwa gharama ya Sh 321 milioni wakati zingegharimu Sh
668 milioni endapo zingenunuliwa nchini.
Katika
taarifa hiyo imebainisha kuwa hospitali hiyo imeweza kupunguza gharama za
uchujaji wa damu (dialysis) kutoka wastani wa Sh 250,000 kwa kila
zamu (session) hadi kufikia Sh171,000.
No comments:
Post a Comment