ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 27, 2016

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE ASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA TICAD VI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kikao cha Mawaziri wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) tarehe 26 Agosti, 2016. Kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Khalid Salum Mohammed na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbelwa Kairuki. 
Balozi Mbelwa akitoa ufafanuzi kwa Mhe. Naibu Waziri kuhusu masuala yatakayojadiliwa kwenye Mkutano huo. 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Amina Mohammed akizungumza wakati wa Mkutano huo. 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Fumio Kishida nae akizungumza wakati wa mkutano wa Mawaziri 
Sehemu ya Wajumbe waliohudhuria mkutano huo 
Sehemu nyingine ya wajumbe 
Picha ya pamoja ya meza kuu. 

MKUTANO WA MAWAZIRI WA TICAD WAFANYIKA JIJINI NAIROBI

Kikao cha Mawaziri kuandaa Mkutano wa Kilele wa Sita wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI) kimemalizika Jijini Nairobi leo ambapo Mawaziri hao wameikubali kwa kauli moja Rasimu ya Azimio la Nairobi na Mpango Kazi wake tayari kwa kuwasilishwa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa ajili ya kupitishwa.

Akihitimisha Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Amina Mohammed amewashukuru Mawaziri wenzake, waandaaji wa kikao hicho na washiriki wote kwa kikao chenye mafanikio na kueleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa agenda zilizojadiliwa zitapitishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kwenye Mkutano wao.

Aidha, alisema kuwa Rasimu hiyo ya Azimio ambalo linazungumzia agenda muhimu tatu ambazo ni Kuhamasisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uendelezaji wa viwanda; Kuboresha sekta ya Afya kwa maisha bora na Kusaidia jitihada za kudumisha amani na utulivu katika jamii linalenga kutatua changamoto mbalimbali na kuiwezesha Afrika kufikia maendeleo endelevu.

Pia, aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuiunga mkono Afrika katika kukamilisha malengo yake ya maendeleo na kwamba mkutano huu wa 6 utaendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano uliopo kati ya nchi za Afrika na Japan.

“Mkutano huu una lengo kubwa moja la kuiwezesha Afrika kufikia maendeleo endelevu kwa kushirikiana na Japan. Hivyo nawapongeza waandaaji na washiriki wote kwa kufanikisha rasimu ya Azimio la Nairobi na ni imani yangu kuwa Azimio hili litapitishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano wao” alisema Mhe. Mohammed.

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Fumio Kishida alisema kuwa Afrika imeendelea kuwa mdau muhimu katika ushirikiano na Japan na kwamba nchi yake inaona fahari kuendeleza ushirikian huo ili kuziwezesha nchi za Afrika kufikia maendeleo endelevu. Pia aliishukuru Serikali ya Kenya kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa TICAD VI na ana matarajio makubwa kuwa utakuwa na tija.

Pia aliongeza kuwa Mikutano ya TICAD ni jukwaa muhimu linaloziwezesha nchi za Afrika na Japan kuangalia vipaumbele mbalimbali katika ushirikiano ili hatimaye kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kuinua uchumi na kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo afya.

Naye Waziri wa Uchumi na Mipango wa Chad, Mhe. Mariam Mahamat Nour ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika alisema kuwa mkutano wa 6 wa TICAD utatoa mwanga kwa changamoto mbalimbali zinazolikabili Bara la Afrika kupitia Azimio la Nairobi mara litakapotishwa na kuanza kutekelezwa.

Kwa upande wa Tanzania Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Mhe. Dkt. Susan Kolimba aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa Mawaziri. Wajumbe wengine waliohudhuria ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohammed na Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali unatarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Agosti, 2016 ambapo moja ya agenda ni kupitisha Azimio la Nairobi. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo.

Mkutano wa Sita wa TICAD unalenga kuiwezesha Afrika katika sekta ya uchumi na uwekezaji ambapo utawashirikisha pia wadau kutoka sekta binafsi zikiwemo Kampuni binafsi zaidi ya 300 kutoka Japan ili kufikia lengo hilo.

-Mwisho-

No comments: