Advertisements

Tuesday, August 16, 2016

VIWANDA VYATAJWA KUCHANGIA UCHAFUZI WA MAZINGIRA YA DAR KWA KIASI KIKUBWA

Jiji la Dar es Salaam linatajwa kwa kukithiri vitendo vya uharibifu na uchafuzi wa mazingira kutokana na uwepo wa viwanda vingi vilivyojengwa pasipo kufuata sheria za mazingira.
Akizungumza katika kipindi cha dakika arobaini na tano kinachorushwa na kituo cha ITV, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira Mh.Luhaga Mpina amesema viwanda vilivyojengwa jijini humo baadhi yake havina miundombinu ya usafirishaji maji taka.
“Dar es Salaam inatisha kwa uchafuzi wa mazingira kwa sababu viwanda ni vingi tena vilianzishwa zamani ambapo havikufuata sheria za mazingira, ” alisema.
Mpina alisema siku za hivi karibuni alifanya ziara katika viwanda 40, Halmashauri 24, na migodi 3 na kubaini kuwa viwanda vingi havitekelezi kwa hiari sheria na utunzaji wa mazingira.
“Katika ziara zangu nimeufunga mgodi mmoja unaofahamika kwa jina la Sunshine Gold Mine uliopo Chunya mkoani mbeya kwa sababu kilifanya uharibifu mkubwa wa mazingira, pia nilifunga kiwanda kimoja, ” alisema.

Alisema iwapo hicho kiwanda na mgodi vitafanya marekebisho na kufuata sheria za mazingira vitafunguliwa.
“jambo hili lisifikiriwe la mchezo watu wanapopata maradhi kutokana na uchafuzi wa mazingira, serikali ndiyo inayowajibika kutoa matibabu hivyo basi haitasita kuchukua hatua kali kwa wanaokiuka sheria ili nchi iwe salama.
Mpina aliongeza kuwa serikali ina mpango wa kupanda miti nchi nzima katika kipindi cha miaka 5 mfululizo kuanzia mwaka huu hadi 2021 ili kuhifadhi mazingira.

No comments: