Advertisements

Sunday, August 14, 2016

WATOTO PACHA WALIOTENGANISHWA WARUDISHWA MUHIMBILI

Watoto pacha waliotenganishwa, Eliud na Elikana Mwakyusa (3) wakazi wa Kasumulu- Kyela, wamesafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) ya kuziba njia za haja ndogo na kubwa zilizotengenezwa kwa dharura ili kuwekewa njia za kudumu.
Akizungumza kwa simu jana akiwa jijini Dar es Salaam, baba mzazi wa watoto hao, Erick Mwakyusa amesema amesafiri baada ya kupata msaada wa fedha kutoka kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela.
Alisema wafanyakazi hao walimpatia msaada huo baada ya kusoma kwenye gazeti la Mwananchi kuhusu matatizo yanayowakabili watoto hao.
Amesema baada ya kupata msaada wa fedha aliwasiliana na daktari wa watoto hao, Dk Zaituni Bokhary ambaye alitaka waende Dar es Salaam.
“Tulifika salama na tumefikia kwa ndugu yetu. Asubuhi hii (jana) tunajiandaa kwenda kuonana na daktari,” amesema.
Ninawashukuru sana kwa msaada wao kwani umeniwezesha kufika Dar es salaam, lakini pia ninawashukuru Mwananchi kwa kufuatilia habari za watoto wangu kwa ukaribu sana, Mola awabariki,’’ alisema Mwakyusa.
Watoto hao waliozaliwa Februari 20, 2013, wilayani Kyela wakiwa wameungana kiunoni na kutenganishwa kwa upasuaji uliofanyika nchini India kwa gharama za Serikali.
Baada ya kufanikiwa kuwatenganisha, watoto hao walitengenezewa sehemu maalumu ya kutolea haja kubwa na ndogo eneo la tumboni na walirejea kijijini kwao Kasumulu Kyela, Februari 27, 2014.
Agosti 2014 watoto hao walifanyiwa upasuaji mdogo Muhimbili na Hospitali ya Rufaa – Mbeya kwa nyakati tofauti wa kuziba njia ya haja kubwa ya muda na kuwatengenezea ya kudumu chini ya Dk Bokhary lakini walitakiwa kufanyiwa upasuaji wa njia ya haja ndogo ili wawekewe ya kudumu.

No comments: