Advertisements

Sunday, August 14, 2016

UTAPELI WA MBAO UNAVYOFANYIKA BUGURUNI

Kama unajenga na umefikia hatua ya kupaua na unadhani Buguruni ndiyo sehemu pekee inayouza mbao nzuri kwa bei poa, fikiria vizuri.
Watu wengi wanaojenga wamekuwa wakifurika eneo la Buguruni Chama au upande wa pili wa kituo cha mafuta, maarufu kama Shell, kununua vifaa vya ujenzi kama mabati, misumari, msasa, vyoo na hasa mbao.
Eneo hilo limejaa mbao ambazo huvuta wateja kirahisi wakijua kuwa ndiyo sehemu muafaka ya kupata mbao zinazouzwa kwa bei nafuu kwa ajili ya kupaua.
Na hilo halina ubishi. Sehemu kubwa ya mbao hizo ni zile zenye ubora na zilizowekwa dawa kitaalamu, lakini unapogeukia suala la bei, hapo ndipo wateja wanapoingizwa mjini.
Vijana wajanja; wenye lugha nzuri; maneno mengi na ushawishi mzuri kwa wateja, ndiyo wanaotawala eneo hilo na ndiyo ambao wanakuwa wa kwanza kuzungumza na mtu yeyote anayeonekana kuwa anataka kununua shehena ya mbao kwa ajili ya ujenzi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwapo kwa matapeli waliojivisha kazi ya udalali. Madalali hao wamejivisha kazi hiyo kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi yanayomilikiwa na wafanyabiashara wengine.
Kazi yao ni kumtapeli mteja kwa kumuuzia mbao chini ya kiwango wanachopima, kumpa mwenye duka stahili yake na wao kuchukua sehemu yao huku wakimuacha mteja akiondoka na mbao pungufu ya kiwango alichoandikiwa na fundi wake.
Na iwapo utaenda na fundi ili asimamie vyema upimaji wa mbao, madalali hao wana uwezo wa kumshawishi aingie kwenye mpango wao na kushirikiana kukuhujumu. Kwa hiyo si ajabu kabla ya kumaliza kupaua, fundi akakwambia mbao hazikutosha na ukalazimika kuongeza nyingine ukijihoji ilikuwaje fundi asipime kwa kadri ya mahitaji ya nyumba.
“Tatizo wateja wengi hutaka mbao kwa bei rahisi wakati haiwezekani,” alisema dalali mmoja kwenye maeneo hayo ambaye ni maarufu.
“Unakuta mbao inayouzwa kwa Sh1,000 kwa mita, yeye anataka apunguziwe hadi Sh800 au Sh750. Sisi tutazitoa wapi?”
Mmoja wa wamiliki wa maduka hayo ya vifaa vya ujenzi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema ukinunua mbao ya bei rahisi ya Sh800 yenye urefu wa futi 18 kwa kutumia madalali ambao wanakuwa wameukata utepe wa kupimia, maarufu kama futi, utajikuta unalipa fedha nyingi zaidi ya ambayo ungeipata kama ungenunua kwa bei halisi ya Sh1,000 kwa mita.
Mteja anayenunua mbao kwa Sh800 kwa mita kwa dalali na ambaye anataka mzigo wa mbao 200, hujikuta analipa Sh3.8 milioni tofauti na ambaye ataenda dukani na kununua bei ya Sh1,000 kwa mita ambaye atalipa Sh3.6 milioni.
Mara nyingi futi za madalali hukatwa na baadaye kuunganishwa zikiwa zimepunguzwa kati ya mita mbili na tatu. Hivyo futi hiyo ikitandazwa kwenye mbao inasomeka urefu wa mita 20 badala ya mita 18.
Kwa mahesabu ya haraka, unachukua Sh800 unazidisha mara mbao 200 unapata Sh160,000,00 kiasi ambacho unakizidisha na futi 24 ambazo zitakuwa zikisoma katika kipimio hicho kilichochezewa, hapo kutakuwa na upungufu wa mita zaidi ya mbili kwenye kila mbao.
Kwa ujumla, mteja atalazimika kulipa Sh3.8 milioni kwa bei hiyo.
Lakini endapo mteja ataenda dukani ambako futi haijachezewa na akanunua mzigo kama huo kwa bei ya Sh1,000 kwa urefu wa mita 18, atalipa Sh3.6 milioni.
Yaani mita 18 zinazidishwa mara mbao 200 na kupata 3,600 kiasi ambacho unazidisha na bei ya mbao Sh1,000 na kupata jumla Sh3.6 milioni.
Taarifa zinasema mara nyingi watu hupenda kuchukua mzigo wa mbao kuanzia 100 na kuendelea kwa ajili ya ujenzi.
Mmoja wa wamiliki wa maduka ya mbao Buguruni, Samwel Jonas alikiri kuwapo kwa utapeli huo Buguruni, akisema mtindo huo unatokea mara kwa mara kwa watu wasiojua vizuri futi hizo.
“Binafsi sifanyi mchezo huu. Ila ni nadra kuujua mtindo huu, kwa sababu mbao haipunguzwi ila kinachopunguzwa ni hiki kipimo,” alisema Jonas. “Kinachowachanganya wateja ni pale wanapoona futi zaidi ya 20 katika mbao badala ya 18 na hivyo kudhani kuwa ameongezewa kumbe anaibiwa.”
Amesema kwa asilimia kubwa, utapeli unafanywa na madalali ambao muda mwingine wanashirikiana na mafundi na baadhi ya wamiliki wa maduka ya vifaa vya ujenzi.
“Ukifika eneo hili, mtu wa kwanza kukutana naye ni dalali,” anasema.
Amesema kwa kiasi kikubwa, madalali wamekuwa wakiharibu biashara ya mbao hapa kwa sababu watu wanakuwa na fikra kuwa maduka yote yana tabia hiyo ya utapeli kumbe ni kinyume.
“Nawasihi wateja wa mbao wakifika Buguruni wahakikishe wanafika ofisini. Wasiishie kuonana na madalali na kuambiwa bei tu,” alisema Jonas.
Mfanyabiashara mwingine, Said Rashid alisema anasikia taarifa hizo za uwapo wa utapeli huo, lakini hajawahi kuona utapeli huo. Hata hivyo, alisema kama vitendo hivyo vipo, havipaswi kufumbiwa macho kwa kuwa vinajenga taswira mbaya kwa maduka ya mbao ya Buguruni.
“Hapa kuna maduka mengi ya mbao. Sijui huu utapeli unafanyika maduka yapi kwa sababu sijawahi kuona. Ila nasikia watu wakizungumzia suala hili,” amesema Rashid na kuwashauri wateja kubeba vipimio vyao wakati wanapokwenda kununua mbao.
Ofisa Daraja la Kwanza wa Wakala wa Vipimo (WMA), Abbas Mtoa alisema utapeli huo ulikuwa ukifanyika kwa wafanyabiashara wa mazuria na walipambana kuwakamata na kuwatoza faini na mchezo huo ulikwisha.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: