Advertisements

Monday, August 1, 2016

WAZIRI MKUU: WAKURUGENZI WATAKAOTOA TAARIFA ZA UONGO KUONDOLEWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitasita kuwaondoa katika nyadhifa zao Wakurugenzi wote watakaoshiriki katika kutoa taarifa za uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao. 

“Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi umekamilika wakati haujajengwa, hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa,” alisema. 


Waziri Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Jumapili, Julai 31, 2016) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Morogoro mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu. 

Alisema alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakurugenzi katika halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatembelea miradi yote inayojengwa katika maeneo yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama thamani yake inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa. 

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Serikali aihitaji Halmashauri kutoa ajira za mikataba kwenye kada zilizopo katika muundo wa ajira hivyo ameziagiza halmashauri zote nchini kufanya mapitio ya watumishi wa mikataba. 

“Tumeruhusu kuajiri kwa mikataba walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha miaka miwili tena kwa waliostaafu. Kuna kada zilizoko katika muundo wa ajira hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba wakiwemo madereva msiwatumikishe kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema. 

Akizungumzia suala la watumishi hewa mkoani Morogoro Waziri Mkuu alisema ni vema wakaendelea kufanya uchunguzi na ifikapo mwisho wa mwezi huu wawe wamekamilisha taarifa na kuanza kuchukua hatua kwa waliohusika kwa waliohusika. 

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe katika taarifa yake aliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu alisema mkoa unaendelea kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuzitaka taasisi zote za Serikali kufanya uhakiki wa mishahara hewa na malipo batili ya watumishi. 

Alisema mkoa umebaini watumishi hewa 315 ambao wameisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 2.132 ambapo timu ya uhakiki bado inaendelea na zoezi hilo na taarifa kamili itatolewa mara kazi hiyo itakapo kamilika. 


IMETOLEWA NA: 
OFISI YA WAZIRI MKUU, 

JUMATATU, AGOSTI 01, 2016.

No comments: