ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 30, 2016

MAJALIWA ATANGULIA DODOMA LEO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa atahamia rasmi Dodoma leo, kama mwanzo wa kutekeleza uamuzi wa Serikali kuhamia makao makuu Dodoma.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili leo mchana.

“Ujio wa Waziri Mkuu ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Julai 25, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kitaifa mkoani Dodoma ambapo aliahidi atahamia Dodoma ifikapo Septemba kama mwanzo wa kutekeleza uamuzi wa serikali kuhamia makao makuu Dodoma,” alisema Rugimbana.

Alisema Waziri Mkuu pia atafanya ziara ya siku mbili katika Manispaa ya Dodoma kuanzia Oktoba Mosi hadi Pili kwa lengo la kukagua hatua mbalimbali za maandalizi ya kupokea ujio wa serikali mkoani Dodoma.

“Atakagua majengo ya serikali, maeneo ya kutolea huduma za afya, kituo cha umeme Zuzu, masoko, chanzo cha maji Mzakwe na maeneo ya viwanda,” alisema Mkuu wa Mkoa na kuongeza kuwa maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mapokezi hayo yamekamilika.

Alisema uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma unampongeza Waziri Mkuu kwa kitendo hicho kikubwa cha kuanza kuitikia na kutekeleza uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli wa kuhamia Makao Makuu mjini Dodoma. Julai 25, mwaka huu akiwa katika sherehe ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa mjini hapa, Waziri Mkuu alisema atahamia Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu na kuwataka mawaziri wote wamfuate.

Aliagiza ukarabati wa nyumba yake iliyopo Dodoma uanze mara moja. Uamuzi huu wa Waziri Mkuu unakuja baada ya Rais John Magufuli kutangaza kwenye Mkutano Mkuu wa CCM mwaka huu kuhamishia shughuli zote za serikali katika Mji Mkuu wa Nchi Dodoma kufikia mwaka 2020.

No comments: