Dar es Salaam. Hatima ya mpango wa Chadema wa maandamano na mikutano mfululizo kupinga kile ilichoeleza ni ukandamizwaji wa demokrasia nchini na kuyapa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), unatarajiwa kutolewa leo.
Awali, maandamano hayo yalipangwa kuanza Septemba Mosi kabla Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kusitisha baada ya kuombwa na viongozi wa dini wakiahidi kukutana na Rais John Magufuli.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema jana: “Naomba mvumilie kesho (leo), tutawaita na kuwaeleza nini tulichoamua juu ya Ukuta.”
Baadaye taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema, Tumaini Makeke ilisema mzungumzaji katika mkutano huo wa waandishi wa habari atakuwa Mbowe ambaye ataambatana na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho.
Julai 27, Chadema ilitangaza Septemba Mosi kuwa siku ya kuendesha harakati za Ukuta ambazo ilisema zinahusisha maandamano na mikutano ili kuishinikiza Serikali kuruhusu mikutano na shughuli nyingine za vyama vya siasa.
No comments:
Post a Comment