Advertisements

Friday, September 30, 2016

MAREKANI YAWATAKA RAIA WAKE KUHAMA DRC

Watu 50 wanadaiwa kuuawa wakati wa maandamano ya upinzani mapema mwezi huu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewaamuru jamaa za raia wake wanaofanya kazi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuondoka nchini humo.

Hii inatokana na kuendelea kwa wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuzuka machafuko ya kisiasa.

Katika wiki za hivi karibuni, maandamano ya upinzani kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais yamekumbwa na vurugu.

Upinzani unasema hatua hiyo ni njama ya Rais Joseph Kabila, ambaye kwa mujibu wa katiba anafaa kuondoka madarakani mwezi Desemba, kuendelea kuongoza.
Marekani yazuilia mali ya maafisa wawili wa DR Congo
'Watu 50 wauawa' maandamano ya upinzani DR Congo
Tume: Uchaguzi hauwezekani mwaka huu DR Congo


Takriban watu 50 wameuawa kwenye makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama mjini Kinshasa.

Maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo pia yamebaki kutokuwa salama, na serikali ya Rais Joseph Kabila imeshindwa kudhibiti hali katika maeneo mengi nje ya miji.

Alhamisi, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Mark Ayrault alinukuliwa akisema kwamba DR Congo imo hatarini ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu rais aliyepo madarakani hataki kung'atuka.

Bw Ayrault alisema hayo alipokuwa akihutubia wanafunzi wa sayansi ya uhusiano wa kimataifa katika chuo kikuu cha Sciences-Po, moja ya vyuo vikuu mashuhuri Ufaransa, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Ufaransa ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikishinikiza kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa kuhakikisha maafikiano kuhusu tarehe ya uchaguzi.

Alisema taifa lake liko tayari kumhakikisha Rais Kabila usalama wake, lakini akaongeza kwamba ni lazima aeleze wazi kwamba hataki kuwania tena madaraka.
Kwa mujibu wa katiba, muhula wa pili wa Rais Kabila, aliyeingia madarakani baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila mwaka 2001, unafaa kumalizika tarehe 20 Desemba.

Mwaka uliopita, watu 12 waliuawa katika maandamao sawa na hayo.
Makao makuu ya upinzani yachomwa DRC

Tangu kujinyakulia uhuru zaidi ya miaka 55, hakuna kiongozi aliyewahi kumkabidhi mrithi wake madaraka kwa njia ya amani.
BBC

No comments: