Advertisements

Tuesday, September 20, 2016

SHAHIDI KESI YA BIL 7/- AELEZA DOLA 'ZILIVYOYEYUKA'

SHAHIDI wa 19 katika kesi ya utakatishaji fedha na wizi wa kutumia mfumo wa mtandao wa kibenki wa zaidi ya Sh bilioni saba inayowakabili wafanyakazi 13 wa Benki ya Exim tawi la Arusha, Thadeud Madawe (37) amedai kuwa yeye ndiye aliyekuwa Mkuu wa Uchunguzi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na aligundua miamala ya dola iliyolipwa katika benki hiyo haikuingia katika akaunti ya mamlaka.
Amesema mahakamani kuwa, aligundua taarifa ya benki ya NCAA haioneshi kuwepo kwa dola 790,000 katika akaunti yake ya dola yenye namba 0310818901 iliyopo katika Benki ya Exim, wakati kampuni za utalii zina taarifa za malipo katika benki hiyo.
Madawe ambaye ni Mhasibu Msaidizi na aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa upotevu wa dola hizo, alikuwa akitoa ushahidi kwa siku mbili jana na leo wakati akiongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Paul Kaduchi mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha na Arumeru, Deusdedit Kamugisha.

Alidai uchunguzi aliofanya kwa kushirikiana na wenzake watatu waligundua kuwa miamala ya dola imelipwa Exim na kampuni za utalii na kupewa karatasi ya malipo iliyogongwa mihuri ya benki hiyo, lakini dola hizo hazikuingia katika akaunti ya NCAA iliyopo katika benki hiyo.
Shahidi huyo amedai kulikuwa na tofauti kati ya taarifa ya benki ya akaunti ya NCAA na karatasi ya malipo za kampuni kadhaa za kitalii zilizolipa dola katika benki hiyo ili kupata huduma ya kitalii kwa wageni wao.
Madawe aliwasilisha mahakamani hapo karatasi hiyo ya benki, taarifa ya akaunti ya NCAA na ripoti yake ya uchunguzi viwe vielelezo katika kesi hiyo na kukubaliwa na mahakama pamoja na kwamba mawakili wa upande wa utetezi, Daudi Haraka na Moses Mhuna kupinga, lakini hoja zao zilitupiliwa mbali.
Amedai alianza kuufanya uchunguzi wa wizi wa dola hizo Oktoba, 2012 na aliwasilisha Polisi baada ya kutakiwa kufanya hivyo na polisi na wakubwa zake wa kazi.
Washitakiwa hao kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2011 hadi 2012 walidaiwa kufanikisha wizi huo kwa kuziibia kampuni mbalimbali za utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia kughushi nyaraka za akaunti ya dola na fedha za Kitanzania na mfumo wa malipo ya kadi.

CHANZO: HABARI LEO

No comments: