Advertisements

Sunday, October 23, 2016

BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU ZANZIBAR YASITISHA KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI VYUO VIKUU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kusimamisha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, hadi hapo serikali itakapojiridhisha na utaratibu mzima wa utoaji wa mikopo hiyo.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi zawadi Mwanafunzi Mahira Baraka Hamadi wa kidato cha sita Skuli ya Biashara Mombasa Wilaya ya Magharibi Unguja akiwa ni mwanafuzi aliyefanya vizuri katika Mtihani wa Taifa Mei mwaka 2016,hafla iliyofanyika jana Ikulu Mjini Unguja.

“Hatutatoa mikopo mwaka huu mpaka hapo tutakapokamilisha kazi ambayo tumeanza kuifanya ya kupitia upya utaratibu wa utoaji mikopo hiyo ili kuhakikisha inatolewa kulingana na mahitaji ya sasa ya nchi na kwa wanaostahili,” alisema Dk Shein.

Akizungumza katika hafla ya utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka 2015 na Kidato cha Sita mwaka 2016, Dk Shein alisema kuwa katika utaratibu wa sasa wapo waliodanganya kupata mikopo na ambao wamekopeshwa lakini wamekuwa wagumu kurejesha mikopo hiyo.

Katika hafla hiyo, ambayo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Usii Gavu, jumla ya wanafunzi 119 waliomaliza kidato cha nne na wengine 50 waliomaliza kidato cha sita, walipewa zawadi kwa kupata daraja la kwanza katika mitihani yao ya taifa.

“Wako waliokejeli matokeo yenu, lakini ukweli ni huo mko 50 wa kidato cha tano mliopata daraja la kwanza na wengine 119 mliofaulu daraja la kwanza mtihani wa kidato cha nne,” alieleza Dk Shein na kuhoji msingi wa kukebehi matokeo hayo.

Aliongeza kuwa ufaulu wa wanafunzi hao, ni sifa kwa Zanzibar na anaamini kwa hatua zinazochukuliwa na serikali kuimarisha miundombinu ya elimu pamoja rasilimali watu kiwango cha ufaulu kitazidi kuongezeka.

“Mnapofanya mitihani sote tunakuwa na wasiwasi, nyinyi wenyewe, walimu, wazazi na sisi serikali kwa kuwa tunaelewa kuwa matokeo yoyote yale ni yetu sote kama ni mazuri ni furaha yetu sote na kama si mazuri ni huzuni yetu sote,” Dk Shein aliwaambia wanafunzi hao.

Dk Shein aliwataka wanafunzi hao kujivunia fursa waliyoipata na kuitumia vyema kujiimarisha kielimu, kwa kuwa haikuwa rahisi kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kuona vijana kutoka familia masikini wanapata fursa za kuingia sekondari kwa makundi.

“Mmepata bahati kubwa serikali yenu imeweka mazingira mazuri ya kupata elimu na haya ni matokeo ya utekelezaji wa ahadi ya Chama cha Afro-Shirazi na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amaan Karume ya kutoa elimu bure itakaposhika madaraka,” Dk Shein alieleza.

Katika hatua nyingine, Dk Shein ametoa wito kwa walimu wakuu kuhakikisha kuwa wanasimamia vizuri walimu katika shule zao pamoja na kuwahimiza wakaguzi wa shule kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Dk Shein alisema; “kumekuwepo na tatizo la usimamizi maskulini, hivyo serikali itatengeneza utaratibu wa kuwapatia motisha walimu wakuu na wakaguzi watakaofanya vizuri kwa kuwa ni dhahiri kuwa walimu wakuu wakisimamia vyema skuli zao na wakaguzi wakaifanya kazi yao ya ukaguzi kwa umakini tutapata matokeo mazuri zaidi.”

Katika salamu zake hizo kwa wanafunzi hao, ambao walisindikizwa na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, pamoja na walimu wakuu wa baadhi ya shule, Dk Shein aliwataka walimu kuongeza ari ya kufundisha na kwamba ni heshima na furaha ya mwalimu kuona mwanafunzi wake anapata matokeo mazuri.

CHANZO: HABARI LEO

No comments: