ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 2, 2016

ENEO LA UWANJA WA YANGA MGOGORO

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji
ENEO la uwanja ambalo Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ameipa klabu hiyo lina mgogoro.

Manji juzi alitoa eneo la hekari 715 lililo ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Gezeulole, Kigamboni kwa ajili ya kujenga uwanja.

Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana zilisema eneo hilo lipo kwenye mgogoro wa ardhi na Kampuni ya mafuta ya Lake Oil. Eneo hilo si lote mali ya Manji bali kuna sehemu nyingine inamilikiwa na Lake Oil.

Akizungumza na HabariLeo jana, mmoja wa wakurugenzi wa Lake Oil, Khalid Hassan maarufu ‘Peter Dau’ alisema ameshangazwa kuona Yanga wamekabidhiwa eneo lote hilo wakati kuna sehemu yao pia.

“Inawezakana Manji amepitiwa kwa kusahau kuwa eneo hilo sio lote lake, kuna sehemu yetu, tumeona leo (jana) kwenye vyombo vya habari imetushangaza,” alisema Hassan.

“Sisi tunawasiliana na wanasheria wetu, vielelezo vyote tunavyo kuwa eneo hilo sisi tumeuziwa, tunachofanya tutatuma wakaguzi wakaangalie mipaka yetu kabla hatua nyingine zaidi za kisheria kuchukuliwa,” alisema.

“Sisi ni wafanyabiashara, naamini kabisa Manji anaelewa sehemu ya uwanja huo sio wake, sidhani kama tutashindwa, natumaini tutalimaliza kwa njia ya amani,” alisema.

Juzi, Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo chini ya Fatma Karume walikabidhiwa eneo litakalojengwa uwanja wa Yanga lililopo Gezaulole, Kigamboni.

Eneo hilo ambalo Manji inadaiwa aliuziwa na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO), kwa upande wa Lake Oil walidai kuwa hawajauziwa na Nafco wameuziwa na mtu mwingine ambaye hata hivyo hawakutaka kumtaja na pia kuweka wazi ukubwa wa eneo ambalo wanadai wanalimiliki.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa Manji baada ya kuuziwa eneo hilo, aliliacha kwa muda mrefu bila kuliendeleza, ndipo watu wengine wakavamia na hata kuuza baadhi ya maeneo.

Jitihada za kumpata Manji hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu na hata Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit hakupatikana kulizungumzia hilo baada ya kutopokea simu pia.

Lakini gazeti hili lilizungumza na mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga Dk Jabir Katundu ambaye ni miongoni mwa waliohudhuria hafla ya makabidhiano juzi ambaye alisema hawajui lolote kuhusu hilo.

“Sisi tumekabidhiwa eneo hatujui kama lina mgogoro lakini Manji kesharudi kutoka safari hivyo tutalipeleka suala hili kujua undani wake na kuangalia namna atakavyolishughulikia,” alisema.

HABARI LEO

No comments: