Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe. Waziri Makamba yuko Mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba, wa tatu kutoka kulia akiangalia chanzo cha maji kilichovamiwa katika Mto Mambogo.
Wananchi wa Kijiji cha Parakuyo wakisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba kabla ya kufanya mkutano wa hadhara kijijini hapo.
Sehemu ya Wananchi wa waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Parakuyo Wilayani Kilosa. Wananchi hao walimweleza Waziri (hayupo pichani) changamoto zinazowakabili juu ya Hifadhi ya mazingira.
Na Lulu Mussa, Morogoro
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January
Makamba ameitaka jamii ya watu wa Parakuyo katika Wilaya ya Kilosa kuishi kwa
amani, uvumilivu na upendo miongoni mwao kwani ndio misingi ya watanzania.
Rai hiyo imetolewa leo katika Mkutano wa hadhara uliojumuisha jamii za wakulima na
wafugaji ambazo zimekuwa na migogoro ya mara kwa mara. Waziri Makamba alizitaka
jamii hizo kuishi kwa amani na kuhifadhi mazingira kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa na jamii hiyo ni kutokuwa na elimu juu ya
mabadiliko ya Tabianchi na athari zake pamoja na kutokuwepo na matumizi bora ya
ardhi.
Waziri Makamba ameuagiza uongozi wa Wilaya na Kijiji kushirikiana pamoja kuunda
kamati ya 'Amani' itakayokuwa na wajumbe kutoka pande zote mbili za wakulima na
wafugaji na viongozi wa madhehebu ya dini ili kutafuta suluhu ya kudumu baina ya
pande mbili ambazo zimekua na migogoro ya mara kwa mara.
"Undeni Kamati hii
mapema na Ofisi yangu itagharamia mafunzo kwa Kamati husika juu ya namna bora ya
kutatua migogoro" alisisitiza Waziri Makamba.
katika jitihada za kukuza uelewa wa masuala ya mazingira na changamoto zake, Waziri
Makamba ameitaka Serikali ya Kijiji kuunda Kamati ndogondogo za Mazingira ambazo
zipo kwa mujibu wa sheria ya Mazingira na kuahidi kuipati mafunzo Kamati hizo ikiwa ni
pamoja na kutengeneza sheria ndogo ndogo zitakazotumika kama nyenzo ya kuhifadhi
na kusimamia Mazingira ya maeneo yao.
Aidha, Waziri Makamba amesema kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ni muhimu
sana na kuitaka jamii ya Parakuyo na Twa twa twa kushiriki kikamilifu katika zoezi la
kuhakiki na kuhesabu mifugo yako ili kubaini ni ardhi kiasi gani inahitajika kwa
wakulima na kiasi gani kwa wafugaji. "ndugu zangu niwasihi, Serikali ina nia ya dhati ya
kuhakikisha kuna kuwa na matumizi bora ya ardhi, hivyo nawashauri mmshiriki
kikamilifu katika zoezi hilo ili kupata uwiano wa idadi ya mifugo na ardhi iliyopo"
Makamba aliongezea.
Awali katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Morogoro Waziri Makamba pia
alitembelea chanzo cha maji na kujionea changamoto za kimazingira katika mto
Mambogo.
No comments:
Post a Comment