Advertisements

Saturday, October 1, 2016

Manunuzi yaitia serikali hasara bilioni 23/-

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Balozi Dk Matern Lumbanga

MAMLAKA ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imefanya ukaguzi wa manunuzi ya umma na kubaini Serikali kupata hasara ya Sh bilioni 23. 41 kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo udhaifu katika kuandaa mipango na kufanya upembuzi yakinifu, uliosababisha ongezeko la gharama ya miradi, maandalizi duni ya mahitaji na udhaifu katika usimamizi wa mikataba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Balozi Dk Matern Lumbanga alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa muhtasari wa ripoti ya ukaguzi kwenye manunuzi ya umma katika mwaka wa fedha 2015/2016 pamoja na taarifa ya uhakiki wa ukaguzi, uliofanyika mwaka wa fedha 2014/2015.
Alisema jumla ya taasisi 70, zilifanyiwa ukaguzi wa ukidhi ulioangalia namna zilivyozingatia sheria na kanuni za manunuzi pamoja na matumizi ya nyaraka za miongozo na mifumo iliyoandaliwa na PPRA.

Alisema kutokana na kufanyika kwa uchunguzi huo, PPRA iliweza kuingilia kati na kufuta mchakato wa zabuni mbili zenye thamani ya Sh bilioni 852.62 baada ya kujiridhisha kuwa serikali isingepata thamani ya fedha.
Pia walibaini serikali inaweza kuokoa Sh bilioni 62.45 kama taasisi husika zitatekeleza mapendekezo yaliyotolewa na PPRA. Pia ukaguzi wa manunuzi ya umma umebaini malipo ya Sh bilioni 1.32 yenye utata, yaliyofanywa na taasisi nne, ambapo wakandarasi walilipwa kwa kazi ambazo hazikufanyika na kwamba taasisi hizo ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, REA, MOI na Mfuko wa Pensheni wa LAPF.
Balozi Lumbanga alisema utafiti huo uliofanyika kati ya Aprili na Septemba mwaka huu ulihusisha taasisi 15 zilizo kwenye kundi la wizara, idara na wakala za serikali, mamlaka za serikali za mitaa 25 na mashirika ya umma 30.
Alitaja taasisi zilizopata alama zisizoridhisha kuwa ni Taasisi ya Uzalishaji (NIP), Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (DART), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Makumbusho ya Taifa, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Bukoba (BUWASA).
Alisema katika taasisi zilizokaguliwa kuangalia uwezekano wa uwepo wa viashiria vya rushwa, asilimia 20 za taasisi hizo ziliashiria uwezekano wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa.
Alitaja taasisi hizo kuwa ni Makumbusho ya Taifa, Ofisi ya Bunge, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Wakala wa Umeme Vijijini (REA), TCRA, DART, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Kwa upande wa ukiukwaji wa sheria na taratibu za manunuzi, PPRA ilifanya uchunguzi wa tuhuma 14 zinazohusu mikataba 49 ya manunuzi inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh trilioni 1.6 na uchunguzi huo ulihusisha taasisi nane.
Alitaja taasisi hizo ni Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Taasisi ya Uhasibu (TIA), Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na TRL.

CHANZO: HABARI LEO

No comments: