Advertisements

Wednesday, October 5, 2016

MWANAMKE AMLEVYWA MLINZI, OFISI SITA ZAIBIWA

MWANAMKE ambaye jina lake halijafahamika alitumika katika wizi wa ofisi sita zilizo kwenye jengo la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Pwani, ambapo vitu mbalimbali viliibwa ikiwemo kompyuta na fedha taslimu ambazo hazijafahamika ni kiasi gani, imebainika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini Kibaha na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, mwanamke huyo alimletea mlinzi, Said Mohamed chipsi na sharubati ambavyo vinadaiwa kuwa na dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Katibu wa CWT mkoa wa Pwani, Nehemia Joseph, amesema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 2 mwaka huu majira ya usiku na watu hao waliiba baada ya kuvunja milango zaidi ya 10 ya ofisi hizo na kompyuta zaidi ya 10.

Joseph amesema mlinzi huyo alipokula chipsi na sharubati alipoteza fahamu na kuwapa nafasi watu hao kuiba bila ya ugumu wowote, baada ya kuvunja milango na kuingia na kuchukua vitu mbalimbali na kutokomea kusikojulikana.

“Kutokana na tukio hilo, jeshi la polisi mkoani Pwani, linawashikilia walinzi wawili wa jengo hilo kutoka kampuni ya Noble Security Tanzania Ltd ya Kibaha, Hamad Kisoki (32) mkazi wa Mailmoja na Said Mohammed (39) mkazi wa Mwanalugali kwa ajili ya upelelezi. Hata hivyo, Kisoki naye alipaswa kuwa lindoni lakini haikufahamika ni kwa sababu gani hakuingia kazini,” alisema.

Alizitaja ofisi zilizopo kwenye jengo hilo la CWT mkoa ambazo zimeibiwa ikiwa ni pamoja na CWT mkoa, CWT wilaya, Beem Financial Services (BFS), Chama cha Wafanyakazi wa hifadhini, mahotelini na majumbani (Chodawu), Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Fedha, Viwanda, Biashara, Huduma na Ushauri (Tuico) na Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania(TCCIA).

“Kwa sasa suala hili liko polisi kwa hatua zaidi na tayari wao wameshakaa na taasisi zote zilizopanga kwenye jengo hilo kwa ajili ya kufanya tathmini ya wizi huo uliotokea na tunashangazwa na mlinzi huyu kununua vyakula kwa mtu asiyemfahamu kwani kwa kufanya hivyo kumesababisha kuwapa mwanya wahalifu na kuleta hasara kubwa kwa ofisi hizo,” alisema.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Bonaventure Mushongi alikiri kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia Oktoba 2 ambapo alisema walipata taarifa majira ya saa 5:00 asubuhi za kuvunjwa kwa jengo hilo kutoka kwa Elizabeth Thomas, katibu wa chama hicho wilaya ya Kibaha.

HABARI LEO

No comments: