Advertisements

Saturday, October 29, 2016

NAIBU KATIBU MKUU, BALOZI SIMBA AITAKA KAMATI YA KUPAMBANA NA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI BINADAMU KUWEKA MIKAKATI YA KUDHIBITI WAHALIFU WA BIASHARA HIYO HATARI NCHINI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya akizungumza na Wajumbe wa Kamati na Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu kabla ya kufungua Mkutano wa siku mbili wa wajumbe hao unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Katika hotuba yake, Balozi Simba aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuweka mikakati imara ya kupambana na uhalifu huo wa usafirishaji wa binadamu ambapo Tanzania ni mojawapo kati ya nchi zilizoathirika na tatizo hilo. Kulia meza kuu ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Vicent Magere, na kushoto ni Katibu wa Sekretarieti kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Separatus Fella. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, Vicent Magere akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya (katikati) kufungua mkutano wa kamati hiyo wenye lengo la kujadili pamoja na kuweka mkakati wa kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu nchini. Kushoto ni Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara hiyo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Naibu Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu, John Makuri akizungumza katika kikao cha kujadili pamoja na kuweka mkakati wa kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu nchini kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, jijini Dar es Salaam leo. Kikao hicho kilifunnguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya (katikati meza kuu). Kulia meza kuu ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, Vicent Magere na kushoto ni Katibu wa Sekretarieti kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Separatus Fella. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Separatus Fella, akiwasilisha mada juu ya Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu na juhudi zilizofanywa na serikali hadi kufikia sasa. Fella alisema Serikali imejipanga kuhakikisha elimu inatolewa kuhusu biashara hiyo na pia kikao hicho kitasaidia kuweka mikakati imara zaidi ya kuendelea kupambana na biashara hiyo haramu. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya (katikati waliokaa), Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, Vicent Magere (kulia waliokaa), Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu kutoka Wizara hiyo, Separatus Fella (kushoto waliokaa) wakiwa na Wajumbe wa Kamati na Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara hiyo, baada ya Naibu Katibu Mkuu kufungua kikao chao cha siku mbili cha kujadili pamoja na kuweka mkakati wa kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu nchini. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Na Felix Mwagara, MOHA
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya amewataka wajumbe wa Kamati ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu kuweka mikakati imara ya kupambana na wahalifu wa biashara hiyo nchini.

Akizungumza kabla ya kufungua mkutano wa wajumbe hao wenye lengo la kujadili na kutengeneza mkakati wa kukabiliana na biashara hiyo, Balozi Simba alisema biashara hiyo imekuwa ikiongezeka duniani na wahalifu wakipata faida ya mabilioni ya fedha kutokana na wahanga, wengi wao wakiwa ni watoto, ambao huporwa utu na uhuru wao.

“Inawezekana wengi wetu hatujakutana na aina hii ya uhalifu, lakini unatokea kila siku duniani kote, na nchi yetu ni mojawapo kati ya nchi zinazoathirika na tatizo la biashara hii haramu,” alisema Balozi Simba na kufafanua;

“Tanzania ni chanzo, njia ya kupitia na pia hupokea wahanga wa biashara hii haramu. Wahanga hawa husafirishwa kutoka maeneo ya vijijini kwenda mijini hapa nchini, wengine husafirishwa kwenda Ulaya, Marekani, Asia na nchi za Kiarabu kama vile Oman na Dubai.”

Alisema watu hao hudanganywa kwa ahadi za kupata ajira nzuri au nafasi za elimu, lakini mwisho wake huishia kunyonywa, kuwa watumwa wa ndani na kufanyishwa kazi kwa nguvu.

Hata hivyo, Simba alisema katika hatua ya kupambana na biashara hii haramu, mwaka 2008 ilitunga sheria ya kudhibiti biashara hiyo hapa nchini, na mwaka 2015 walikamilisha kazi ya kuandaa Kanuni za kutekeleza sheria hii. Aliongeza kuwa, sheria hii ndiyo ilipelekea kuundwa kwa Kamati na Sekretariet ya kupambana na biashara hiyo haramu ya usafirishaji binadamu.

“Na leo Kamati na Sekretarieti mnakutana hapa kwa lengo hilo la msingi, kwamba mnafanya tathmini ya utendaji wenu tangu mwaka 2012 hadi sasa ili kubaini wapi mlifanya vizuri na wapi hamkupata mafanikio mliotarajia. Tathmini hii itawawezesha kuweka mikakati thabiti ya kuzuia na kupambana na tatizo hili hapa nchini,” alisema Balozi Simba.

Simba alisema anajua wana mafanikio mengi ambayo Kamati hiyo wameyapata katika utendaji wao tangu kuanzishwa ikiwemo baadhi yake ni pamoja na kuandaa Kanuni za sheria ya kupambana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa kupambana na biashara hiyo na kuimarika ushirikiano wa kiutendaji baina yao na idara zingine za serikali, pamoja na Mashirikia yasio ya kiserikali na ya Kimataifa mfano Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Wahamaji (IOM).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, Vicent Magere, alisema kikao hicho kinawahusisha Wajumbe wa Kamati na Sekretarieti kutoka Bara na Visiwani ambapo wanakutana kwa mujibu wa sheria ambapo wanapaswa kukutana mara tatu au nne kwa mwaka.

“Lengo la kukutana ni kufanya tathmini ya utendaji ili kubaini ni wapi tulifanya vizuri na wapi hatukufanya vizuri. Kikao hiki pia kinatupatia fursa ya kupanga mikakati ya utendaji ili hatimaye tuweze kuboresha zaidi utendaji wetu,” alisema Magere.

No comments: