POLISI Mkoa wa Pwani inawashikilia watoto 22 wa madrasa iitwayo Arahma iliyopo Kata ya Nianjema Tarafa ya Mwambao wilayani Bagamoyo kwa tuhuma za kujifunza namna ya kutumia milipuko.
Mbali ya kuwashikilia watoto hao, waliokamatwa walipokuwa wakijaribu kukimbia, kati yao 16 ni wa kike na sita wa kiume kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo, pia inamshikilia mwalimu wao, Ashura Said (47) mkazi wa Kimarang'ombe Kata ya Nianjema kwa kwa tuhuma za kuendesha mafunzo ya kigaidi kwa watoto.
Kwa mujibu wa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Bonaventura Mushongi, Ashura Said mbaye ni mwalimu wa madrasa iitwayo Arahma, na alikamatwa wakati wa msako wakushitukiza uliofanywa na makachero wa jeshi hilo.
Mushongi amesema mtuhumiwa alikamatwa Oktoba Mosi saa tisa alasiri kutokana na taarifa zilizokuwa zimetolewa na raia wema juu ya mwenendo wa mwalimu huyo wa madrasa .
Alisema baada ya kumfanyia upekuzi, walikuta bomu moja la moshi lenye namba G2020c.SS-STCS katika makazi yake.
“Katika uchunguzi wa awali tumeweza kubaini kuwa makazi hayo yanamilikiwa na Taasisi ya Kiislamu iitwayo AKHA LAAGUL ISLAM iliyosajiliwa kwa lengo la utoaji huduma kwa watoto yatima kwa watoto kutoka maeneo mbalimbali kama vile Dar es Salaam, Handeni Tanga, Mlandizi na Bagamoyo kwa Mkoa wa Pwani, lakini badala yake wamekuwa wakitumika kwa mafunzo yasiyofaa kwa watoto wa kituo hicho,” alisema Kamanda Mushongi.
Katika tukio lingine, watu wasiofahamika wamevamia Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Kimanzichana Kusini na kumuua mtu mmoja na kumjeruhi mwingine kwa risasi.
Kamanda Mushongi alisema tukio hilo ni la juzi saa 11 alfajiri katika Kitongoji cha Ukwama Kata ya Kimanzichana Tarafa ya Mkamba Wilaya ya Mkuranga, wakati aliyeuawa akiwa anajaza fomu za mkopo wa Benki ya Akiba Commercial Bank (ACB) ni Bakar Said (45) mkazi wa Kimazinchana Kusini.
“Watu wawili walivamia ghafla wakiwa na silaha mbili na kuanza kuwafyatulia risasi ambazo zilimpiga Bakari na kutoweka kusikojulikana wakitumia pikipiki,” alisema Mushongi.
Alisema mtu huyo aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani upande wa kulia na kutokea chini ya bega la kushoto mgongoni. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga na utakabidhiwa kwa ndugu zake mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha, katika tukio hilo, Omary Ally (55) ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kimanzichana Kusini, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi kwenye mkono wa kushoto na amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa matibabu.
“Katika eneo la tukio kumekutwa maganda mawili ya risasi yanayotumika kwenye silaha ya SAR/SMG na tunapenda kuwahakikishia wananchi wote usalama wao na kwamba tutahakikisha tunapambana kwa nguvu zetu zote na wale wote wenye nia ya kuwatia hofu wananchi hawataweza kufanikiwa katika mipango yao waliodhamiria," alisema.
No comments:
Post a Comment