Mkuu wa Bandari ya Kigoma Bw. Athuman Mwaibamba akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani alipoitembelea bandari ya Kigoma kukagua utendaji kazi wa bandari hiyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo kwa wafanyakazi wanaopakia na kushusha mizigo katika bandari ya Kigoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akisikiliza changamoto zinazowakabili abiria wanaotumia treni ya reli ya kati katika stesheni ya Kigoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akipata ufafanuzi kutoka kwa Kaimu mkuu wa Shirika la Posta Mkoa wa Kigoma Bw.Juma Kaungenge wakati alipokagua huduma za posta katika mkoa huo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa viongozi wa uwanja wa ndege na Mamlaka ya anga Mkoani Kigoma namna ya kuhudumia ndege ili kuvutia idadi ya abiria.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akiwaaga viongozi na
watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mkoani Kigoma mara baada ya kuzindua safari za
ndege Bombadier Q400 toka Kigoma kwenda Dar es salaam. Picha na Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano -WUUM
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewataka wakazi wa mikoa ya Kigoma,
Katavi na Rukwa kuwekeza katika biashara na vivutio vya utalii ili kunufaika na
fursa ya ujio wa Ndege mpya za Shirika la ndege Tanzania (ATCL) katika kanda
hiyo.
Akizungumza wakati wa
kuzindua usafiri wa ndege ya ATCL kutoka Kigoma kwenda Dar es salaam Eng.Ngonyani
amesema Serikali itahakikisha inaufufua ukanda wa magharibi mwa Tanzania kwa kuimarisha
barabara za lami na kuwa na safari za ndege za uhakika ili kuvutia watalii
kutembelea vivutio hivyo na hivyo kukuza uchumi wa mikoa hiyo.
“Kwa kuanza ATCL
itakuwa na safari nne kwa wiki kuja Kigoma na idadi ya abiria ikiwa ya kutosha
tutaziongeza ili kuwawezesha wasafiri na wadau wengine wa utalii kufika Kigoma
kwa urahisi”, Amesema Eng. Ngonyani.
Amewataka wafanyakazi
wa ATCL na viwanja vya ndege nchini (TAA), kuwa wabunifu ili kuvutia abiria
wengi na hivyo juhudi za Serikali za kuiunganisha nchi kwa usafiri wa anga zifanikiwe katika muda mfupi.
“Serikali tutaendelea
kuongeza ukubwa wa uwanja wa ndege wa Kigoma na Mpanda na kutoza gharama nafuu
ili kuwezesha ndege nyingi kutua katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na kuwezesha
abiria na watalii wengi kunufaika na usafiri wa anga,”. Amesisitiza Eng. Ngonyani.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri Ngonyani amemuagiza Mkuu wa Stesheni ya reli Kigoma Bw. Ally Shamte na Mkuu
wa Bandari ya Kigoma Bw. Athumani Mwaibamba kutengeneza mkakati wa pamoja
utakaowezesha bandari ya Kigoma kupata mizigo mingi kutoka katika nchi za
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi na hivyo kuwezesha biashara
ya uhakika kufanyika katika bandari hiyo.
“Angalieni soko
lilivyo na jinsi soko linavyobadilika,
hakikisheni mnaongeza wateja na kuongeza ubunifu ili watu wavutike kutumia
bandari yetu”. Amesisitiza Eng. Ngonyani.
Naibu Waziri huyo
amesema Serikali itaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya reli na
bandari hivyo kazi ya watendaji iwe ubunifu wa kibiashara ili kuiwezesha
Serikali kupata faida.
Mwenyekiti wa taasisi
zilizo chini ya wizara ya ujenzi,uchukuzi na mawasiliano ambae pia ni Meneja wa
Wakala wa Barabara mkoa wa Kigoma (TANROADS) eng. Narcis Choma amemhakikishi Naibu
Waziri Ngonyani kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya mkoa wa
Kigoma ili kukuza uchumi wa watu wa kanda ya magharibi.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment