Advertisements

Friday, November 25, 2016

MCHUNGAJI ANTHONY LUSEKELO (MZEE WA UPAKO) ANADAIWA KUMFANYIA FUJO JIRANI YAKE HUKU AKIWA AMELEWA

Mtu huyo anayedaiwa kuwa Mzee wa Upako, anaonekana amevalia shati la rangi ya bluu na suruali nyeusi, anasikika akimfokea mtu aliye ndani na kumuonya asikutane naye.
Katabazi aliithibitishia Mwananchi kuwa taarifa hiyo iliyosambaa kuhusu Mzee wa Upako ni yake na kwamba alimkuta mchungaji huyo asubuhi eneo la Kawe Beach anakoishi akiwa anawatolea maneno makali watu waliokuwa ndani ya uzio wa nyumba, akidai kuwa wanamdharau.
Alisema kwa mujibu wa watu saba aliowakuta kwenye eneo la tukio, mchungaji huyo alikuwa akirejea nyumbani kwake asubuhi hiyo akionekana kutokuwa katika hali ya kawaida.
Lakini kabla ya kufika nyumbani alisimamisha gari lake mbele ya geti la nyumba ya jirani yake na kuanza kuwatolea maneno hayo kwa madai kuwa wamekuwa wakimkebehi yeye kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ni mlevi.
“Nilimsihi sana hadi saa moja asubuhi nikimwomba anisikilize, aache kutukana, kutoka katika eneo la nyumba ya watu kwa sababu yeye ni mtumishi wa Mungu anajidhalilisha ,” alisema Katabazi.
Katabazi alisema mchungaji huyo hakumsikiliza.
Katabazi, ambaye alidai kuwa wakati huo Mzee wa Upako hakuonekana kuwa katika hali nzuri, alikubali kwenda nyumbani.
Hata hivyo, Katabazi alisema baada ya muda mfupi Mzee wa Upako alirudi kwenye nyumba hiyo na kuanza tena kutoa maneno hayo.
Katabazi alisema kwa kuwa kulikuwa kumeshapambazuka taarifa zilianza kusambaa, askari wa kituo cha polisi cha Kawe walifika eneo hilo na kumchukua.
Lakini Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hana taarifa za kukamatwa kwa Mzee wa Upako.
Wakati taarifa zinadai kuwa baadaye alichukuliwa na askari wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro hakutaka kuzungumzia suala hilo na kuahidi kutoa taarifa ya tukio hilo leo.
Mlinzi wa nyumba ambayo Mchungaji Lusekelo alikutwa akitoa maneno hayo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema alifika asubuhi majira ya saa 11:00 na kuegesha gari barabarani kisha kuanza kufoka.
Baada ya kufoka mtu mmoja alitoka na kumuita kwa kutumia cheo cha mchungaji, lakini alijibiwa “mchungaji hukohuko”, na kuendelea kufoka, jambo lililofanya walinzi kupiga simu polisi.
Alisema polisi walifika muda mfupi baadaye na kutaka kujua sababu za mchungaji huyo kuitaarifu polisi kama ana matatizo na jirani yake, lakini akawa anatoa maelezo ambayo walishindwa kuyaelewa na hivyo kuondoka naye.

Mke wa mchungaji huyo, Happiness Ngasala aliiambia Mwananchi kuwa mchungaji huyo alikuwa nyumbani kwake.
“Mume wangu yupo nyumbani hapa. Hizo taarifa hazina ukweli wowote,” alisema.
Kuhusu madai ya kutoa maneno nayo, Ngasala alisema: “Hata huo waraka si wa kweli. Mchungaji hawezi kutoa maneno kama hayo.”
Ngasala, ambaye alithibitisha kwamba mume wake yupo nyumbani alipoombwa ampe Mzee wa Upako simu ili mwandishi azungume naye, alisema apigiwe kwenye simu yake.
Mwandishi alipomwambia kwamba mchungaji huyo amepigiwa simu yake lakini hajapokea, alisema mume wake hajakamatwa na kwamba kuna kinyozi alifika kwa ajili ya kumnyoa nywele, hivyo apigiwe baadaye.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: