ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 25, 2016

TIMU LIPUMBA, MAALIM ZATWANGANA MAHAKAMANI

KATIKA hali isiyo ya kawaida, wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), jana waligeuza Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kuwa ukumbi wa masumbwi baada ya kutwangana baadhi yao walipojaribu kumzuia Profesa Ibrahim Lipumba kuingia kusikiliza kesi inayomhusu.
Watu hao ambao walikuwa wamevaa sare za chama hicho, walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili, moja likiwa kwa Profesa Lipumba, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Upande mwingine ulikuwa wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chama hicho, Abdallah Khatau, wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ambao wamefungua kesi ya kupinga uenyekiti wa kutambuliwa na Msajili.
Jana saa 2:45 asubuhi, wafuasi wa pande zote mbili katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, zilikuwa zimetanda kwenye korido za mahakama hiyo wakisubiri kuingia chumba cha korti kusikiliza shauri hilo.
Hata hivyo, baada ya mawakili kuingia katika ofisi ya Jaji Sekiet Kihio kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo, baadhi ya wafuasi hao walisimama mlangoni kumzuia Profesa Lipumba na watu wake wasiingie kwenye chumba hicho.
“Huwezi kuingia ndani hadi mawakili waingie", "kaja kufanya nini wakati kesi haimuhusu," "ondoka Lipumba…,” walisikika wakisema baadhi ya wafuasi hao.
Hatua hiyo ilisababisha wafuasi wa Prof. Lipumba kuanza kupiga kelele huku wakitaka wenzao wanaomzuia kutoka mlangoni ili aweze kuingia kusikiliza kesi hiyo.
Tukio hilo lilikuwa kama sinema baada ya timu ya Prof. Lipumba kumnyanyua juu juu mtu aliyesimama mlangoni kumzuia mlalamikiwa huyo kuingia mahakamani na baadaye walimshushia kipigo huku moja wao akisikika akisema “mnataka kuharibu kesi, toka hapa mlangoni na usirudi tena."
Wakati 'sinema' hiyo ikiendelea hakukuwa na askari eneo hilo hivyo kufanya fujo hizo zidumu kwa zaidi ya nusu saa mpaka askari polisi na magereza walipofika na kufanikiwa kuwatuliza wafuasi hao na Prof. Lipumba kuingia kusikiliza kesi yake.
Ndani ya chumba cha mahakama, Jaji Kihio aliwalaumu mawakili wa pande zote mbili kwa kuonyesha utovu wa nidhamu mahakamani hapo na kwamba hawakustahili kufanya hivyo.
“Nasikitika sana kwamba ninyi wote ni watu wazima inakuwaje mnaanzisha vurugu wakati kesi yenu imepangwa kwa ajili ya kutajwa?
“Kesi yenu inatajwa kwa dakika tano, nashangaa mnaamua kupigana, mawakili siku nyingine mnatakiwa kutoa taarifa kuwa mmekuja na wafuasi wengi ili twende mahakama ya wazi,” alisema Jaji Kihio.
Wakili wa Mlalamikaji, Juma Nassoro, aliomba Jaji Kihio ajitoe kusikiliza kesi hiyo.
Alidai kwamba wamewasilisha pingamizi dhidi ya majibu ya walalamikiwa kwa madai kwamba yana upungufu wa kisheria.
Alidai kuwa viapo vya walalamikiwa vina upungufu wa kisheria na kwamba vilitoa maelezo ya uongo pamoja na muapaji kuweka maelezo ya kuambiwa.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata, aliwasilisha pingamizi la awali kwamba mahakama hiyo haijatoa kibali cha kufungua kesi dhidi ya walalamikiwa.
Jaji alisema kuhusu suala la kuombwa ajitoe bado hajapokea barua kutoka upande wa mlalamikaji na kwamba akipokea barua hiyo atatoa uamuzi siku ya kusikiliza pingamizi Desemba 6.
Mbali na Msajili, walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ya madai namba 23/2016 ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof. Lipumba na wanachama wengine 11 wa CUF.

No comments: