Advertisements

Monday, November 14, 2016

MWENYEKITI JELA KWA KUTUMIA VIBAYA MADARAKA

MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh 200,000 aliyekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Igogo, Kata ya Nanga, Elinkaila Isaya baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga, Ajali Millanzi alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umemuona aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji ana hatia hivyo atalipa faini Sh 200,000 au akishindwa kulipa atakwenda jela miaka miwili. Hata hivyo, mshtakiwa alilipa na kuachiwa huru na mahakama huku washtakiwa watatu wakiachiwa huru.

Awali, ilidaiwa mahakamani na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Nzega, Aidani Samali mbele ya Hakimu Millanzi, kwamba Oktoba 13, 2014 akiwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Igogo pamoja na viongozi wengine wa Serikali ya Kijiji akiwemo Mtendaji wa kijiji hicho, Henry Masanja na wajumbe wawili wa Kamati ya Fedha, Boniphace Jagadi na Helena Maduhu walitumia vibaya madaraka yao.

Kwamba walishindwa kujenga matundu ya vyoo 12 katika shule ya msingi Igogo na kujipatia fedha Sh milioni 5.1 kwa manufaa yasiyostahili.

Mwendesha Mashitaka huyo wa Takukuru aliendelea kuiambia Mahakama kuwa shitaka la pili Novemba 24, 2014 mshitakiwa na wenzake walishindwa kujenga choo cha ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho na kujipatia fedha Sh milioni 3.1 kwa manufaa yasiyostahili.

Aidha, shitaka la tatu ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kati ya Oktoba 13 na Novemba 24, 2014 jumla ya fedha Sh milioni 8.2 walizitumia kwa maslahi yao binafsi. Mwendesha Mashitaka alibainisha shitaka la nne kuisababishia serikali hasara katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.

Alidai washtakiwa walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007 inayozuia kutenda makosa kama hayo.

Baada ya kusomewa mashitaka, washtakiwa walikana shitaka ambapo upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi 10 ambapo wote walitoa ushahidi mahakamani dhidi ya washtakiwa.

HABARI LEO

No comments: