Advertisements

Monday, November 14, 2016

UMEME NCHI NZIMA

KUANZA kwa Utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (Turnkey III) ambao unafanywa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) utaifanya Tanzania Bara yote kuwaka umeme ndani ya miaka mitano.

Mradi huo utakaotekelezwa ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha, utaviunganisha vijiji vyote vya Tanzania Bara ambavyo havijapatiwa huduma ya umeme kuunganishiwa nishati hiyo.

Wakati akiahirisha Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema mradi huo utapeleka umeme katika vijiji 7,873 viliyoko katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara. Kwa mujibu wa Majaliwa, vijiji hivyo vitaanza kuunganishiwa umeme kuanzia mwaka huu wa fedha 2016/17.

Kati ya vijiji hivyo, vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi kutokana na nishati jadidifu. Waziri Mkuu alisema REA inafanya hivyo kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuvipelekea umeme kwa gharama nafuu kwa sasa.

Kwa mujibu wa takwimu za REA, hadi kufikia sasa jumla ya vijiji 4,395 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara sawa na asilimia 36 tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme.

Kama Tanzania ina vijiji 12,268, vijiji ambavyo vimeunganishiwa umeme hadi sasa ni vijiji 4,395, vijiji viliyokuwa vimebaki bila kuunganishwa na huduma ya umeme ni 7, 873 ambavyo Waziri Mkuu ametangaza kuwa vitaunganishiwa umeme ndani ya miaka mitano.

Majaliwa alisema mpango huu wa tatu utaongeza wigo wa usambazaji umeme katika maeneo ambayo hayakufikiwa na miradi ya REA Turnkey Phase I na II. Alisisitiza kuwa ili kutekeleza miradi hiyo kwa kasi zaidi, Serikali ya Awamu ya Tano katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 iliongeza fedha za kupeleka umeme vijijini kutoka Sh bilioni 357.117 zilizotengwa mwaka 2015/16 hadi Sh bilioni 587.61 mwaka 2016/17.

"Hadi kufikia mwezi Oktoba, serikali imetoa Shilingi bilioni 109.8 kwa ajili ya Mfuko wa Nishati Vijijini kutoka kwenye vyanzo vya fedha za ndani. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 100.4 ni tozo ya mafuta na Shilingi bilioni 9.4 ni tozo ya umeme,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa zabuni za kupata makandarasi wa kutekeleza mradi huu zilitangazwa 1 Agosti, 2016,” .

Alisema kwa sasa REA inaendelea na uchambuzi wa zabuni hizo na taratibu zote za mradi huo zimepangwa kukamilika mwezi Januari, 2017.

“Natoa rai kwa viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo waheshimiwa wabunge kuwahamisha wananchi katika maeneo yao kutumia fursa ya kuunganishiwa umeme wakati makandarasi wakiwa kwenye maeneo ya miradi. Katika kipindi hicho bei ya kuunganisha umeme ni Sh 27,000 tu," alisema Majaliwa.

Mikakati ya REA Kwa mujibu wa REA, usambazaji wa umeme wa Gridi ya Taifa utahusisha kufikisha umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme wa gridi, kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme katika maeneo yenye miundombinu ili kufikisha umeme kwenye vitongoji ambavyo havikufikishiwa umeme kwenye mradi wa Turnkey II utakaotekelezwa kama sehemu ya Turnkey III.

Rea katika taarifa yake iliyoko kwenye tovuti ilifafanua kuwa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa nishati jadidifu kwenye visiwa na maeneo ya vijijini yaliyo mbali na gridi itakayotekelezwa na sekta binafsi kwa ruzuku kutoka Mfuko wa Nishati Vijijini.

Rea inaeleza kuwa miradi ya kusambaza umeme wa gridi itagharimu Sh bilioni 7,000. Kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh bilioni 4,000 ni kwa ajili ya kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikishiwa umeme katika mikoa na wilaya zote; na kiasi cha Sh bilioni 3,000 kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo yameshafikiwa na miundombinu ya umeme, lakini baadhi ya vitongoji na taasisi bado havijafikiwa na umeme.

Tovuti hiyo ya REA inaeleza kuwa gharama halisi zitabainishwa baada ya zabuni kupokelewa na kuchambuliwa. Fedha hizi zitatoka kwenye Bajeti ya Maendeleo ya Serikali kila Mwaka; tozo kwenye petroli na mafuta ya taa, tozo ya umeme na michango ya Washirika wa Maendeleo.

Pia REA ilisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu kwa vijiji 176 vilivyo mbali na gridi utaanza katika Mwaka wa Fedha 2016/17 na itatekelezwa na sekta binafsi kwa ruzuku kutoka serikalini kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo.

Miradi yote chini ya Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu itatekelezwa na makandarasi binafsi kwa utaratibu wa Turnkey kwa usimamizi wa pamoja kati ya REA, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Amana.

HABARI LEO

No comments: