TAREHE 27-28 NOVEMBA, 2016
1. Mheshimiwa Idriss Deby Itno, Rais wa Jamhuri ya Chad na Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika atakuwa na Ziara ya Kikazi nchini Tanzania tarehe 27-28 Novemba, 2016.
2. Mheshimiwa Rais Deby atawasili tarehe 27 Novemba, 2016 na kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mjini Dar es Salaam saa 8.00 mchana na kulakiwa na Mwenyeji wake Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania. Aidha, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Tanzania watakuwepo Uwanja wa ndege katika mapokezi hayo.
3. Akiwa hapa nchini, Mheshimiwa Rais Deby na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakuwa na mazungumzo rasmi Ikulu, ambapo watapata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika kwa ujumla.
4. Mheshimiwa Rais Idriss Deby ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa Mwaka 2016-2017, kipindi ambacho Umoja huo umeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili bara letu, zikiwemo ugaidi, amani na usalama, na changamoto za maendeleo Barani Afrika.
5. Ujumbe wa Rais huyo pia unawajumuisha Mke wa Rais Mama Hinda Deby Itno, Mheshimiwa Moussa Faki Mahamat, Waziri wa Mambo ya Nje, Mtangamano wa Afrika, na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chad na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Chad.
Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI,
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
27 NOVEMBA, 2016
No comments:
Post a Comment