ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, December 31, 2016

HOSPITALI YA MISHENI SIKONGE YAKABILIWA NA TATIZO LA KUNGUNI

Image result for SIKONGE
Na Mussa Mbeho Sikonge

HOSPITALI ya Misheni wilayani Sikonge Mkoani Tabora inayomilikiwa na kanisa la Moravian Tanzania inakabiliwa na tatizo sugu la uwepo wa wadudu wengi aina ya kunguni hali inayohatarisha afya za wagonjwa wilayani humo.

Hayo yamebainishwa jana na Mganga Mkuu Msaidizi wa hospitali hiyo Dk John Buswelu alipokuwa akitoa taarifa ya hospitali kwa Mkuu wa wilaya hiyo Peresi Magiri aliyeambatana na Mbunge wa jimbo hilo Joseph Kakunda, Mwenyekiti wa halmashauri Peter Nzalalila na Wataalamu wa
halmashauri hiyo.

Alisema tatizo la uwepo wa kunguni hao katika Hospitali hiyo Teule ya wilaya lilianza tangu mwaka 2013 na jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na wataalamu wa wadudu bila mafanikio yoyote.

Alisema dawa pekee iliyokuwa na sumu kali duniani kote ya kuua wadudu hao ya DDT ilishapigwa marufuku tangu miaka ya 1970 kwa sababu ya kuwa na athari kubwa kwa mazingira (hali ya hewa).

Alibainisha kuwa wadudu hao chakula chao kikuu ni damu na mtu aliyeumwa hujisikia kuwashwa na wengine kuvimba na kuongeza kuwa katika hospitali hiyo wamekuwa sugu kwa sumu na baadhi ya dawa kwa sababu wana ngozi nzito na mayai yao yana mfano wa plastiki
inayowasaidia kujilinda na dawa yoyote.

Alitaja madhara ya wadudu hao kuwa ni wagonjwa kutopata usingizi kutokana na usumbufu wanaopata usiku kucha, kupata upele unaoitwa kitaalamu tropical pruritis, homa ya kunguni na watumishi kupata madhara ya kisaikolojia.

Licha ya madhara hayo wanayopata wagonjwa katika hospitali hiyo Dk Buswelu aliongeza kuwa uwepo wao pia ni aibu miongoni mwa jamii hususani katika eneo la hospitali kwani mgonjwa analetwa akiwa na shida nyingine na kujikuta akipata tatizo jingine.

Alitaja chanzo kikuu cha wadudu hao kuwa ni uchafu na wakati mwingine baadhi ya wagonjwa huja nao kutoka nyumbani kwao na kuwaeneza katika vitanda vya hospitalini.

Kilio cha wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo kimesikika, Mbunge wa jimbo hilo Joseph Kakunda ametoa kiasi cha sh 850,000/- kutoka mfukoni mwake kwa ajili ya kutokomeza kunguni hao hatua ambayo imeleta faraja kubwa kwa halmashauri ya wilaya hiyo, uongozi wa hospitali na
wana Sikonge wote.

Mkuu wa wilaya hiyo Peresi Magiri na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Peter Nzalalila wamempongeza sana mbunge kwa kujitoa kwa moyo mmoja kumaliza tatizo hilo kwani lilikuwa changamoto kubwa kwa wakazi, wagonjwa na uongozi wa hospitali hiyo.

Aidha waliahidi kuwa halmashauri ya wilaya hiyo itashirikiana na uongozi wa hospitali ili kuhakikisha changamoto nyingine zilizopo zinapatiwa ufumbuzi haraka.

No comments: