JESHI la Polisi katika Kanda Maalumu Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 586 kwa makosa mbalimbali katika msako uliofanyika kwa siku kumi kuanzia Novemba 22 mwaka huu.
Hayo yalisemwa jijini humo na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.
Alisema watuhumiwa hao wamekamatwa maeneo mbalimbali kwa nyakati tofauti kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba usiku na kuiba, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kubughudhi abiria, wizi wa magari, shambulio la aibu na la kawaida, kutengeneza, kuuza na kunywa pombe haramu ya gongo pamoja na uvutaji bangi.
Aliongeza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya operesheni iliyofanyika maeneo ya Buguruni na Magomeni ambapo walikamatwa jumla ya watuhumiwa 257, walikamatwa kwa makosa mbalimbali na jumla ya lita 405 za Pombe haramu za gongo zilikamatwa, mitambo miwili ya kutengenezea gongo na bangi.
Kamanda Sirro alisema baadhi ya watuhumiwa hao walikutwa na silaha ndogo ndogo za kufanyia uhalifu kama visu, nyembe, bisibisi. Katika tukio jingine , Polisi Kanda Maalum Dar es salaam kupitia kikosi kazi cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha, mnamo Novemba 29, mwaka huu majira ya saa nne na nusu Kijichi Neluka Mbagala lilifanikiwa kukamata gari lililobeba mali za wizi.
Sirro alisema gari hilo lilikamatwa baada ya majambazi watatu wakiwa na gari Toyota Noah lenye rangi ya fedha lililosajiliwa kwa namba za usajili T 129 DDS, kuvamia baa moja inayofahamika kwa jina la Whatsapp na kuvunja, kisha kuiba vitu mbalimbali vikiwemo seti ya televisheni aina ya Samsung, king’amuzi kimoja cha startimes kimoja, radio moja, spikambili aina ya Sony, na katoni tatu za glasi.
No comments:
Post a Comment