Wananchi wa kijiji cha Jengwe kata ya Kitanga katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wamewalalamikia viongozi wa wilaya ya Kasulu kwa kupora zaidi ya ekari mia nane za mashamba na kusababisha zaidi ya kaya mia tano kukosa maeneo ya kilimo na ufugaji.
Wakitoa malalamiko yao kwa waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mh William Lukuvi, wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakilima mashamba yao lakini serikali ya wilaya imekuja na kuyachukua kwa nguvu na kusababisha zaidi ya kaya mia tano kukosa maeneo ya kilimo ambapo wameiomba serikali kuupatia suluhisho mgogoro huo.
Mkuu wa wilaya ya Kasulu kanali Martin Mkisi amesema mashamba hayo yallichukuliwa kutokana na mpango mahsusi wa kilimo kwanza ambapo lengo lilikuwa kuwapatia vijana mashamba, mpango ambao haukufanikiwa na kusababisha watu kujichukulia mashamba hayo kinyume cha utaratibu.
Kutokana na mgogoro huo waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mh. William Lukuvi ameagiza polisi na idara ya ardhi kufanywa uchunguzi wa suala hilo haraka.
No comments:
Post a Comment