Advertisements

Friday, December 16, 2016

MWANZILISHI WA JAMIIFORUMS AFIKISHWA MAHAKAMANI, AKOSA DHAMANA

Mwanazilishi wa Mtandao wa JamiiForums aliyekamatwa na Polisi kuanzia juzi Maxence Melo, leo amefikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu Jijini Dar es Salaam leo asubuhi na kusomewa mashtaka matatu.

Melo amefikishwa mahakamani leo ikiwa ni baada ya sitofahamu kubwa iliyokuwa imetanda kuhusu kosa hasa la kukamatwa kwake ambapo tangu alipokuwa amekamatwa zaidi ya saa 24 zilizopita hakuwa amefikishwa mahakamani huku Polisi wakiwa wamefanya upekuzi ofisini kwake na nyumbani.

Maxence Melo amepandishwa kizimbani leo na kusomewa mashtaka matatu yanayomkabili likiwemo la kumiliki na kuendesha tovuti ambayo haijasajiliwa hapa nchini Tanzania (JamiiForums).


Mashtaka mengine ni kuzuia na kuharibu taarifa ambazo Jeshi la Polisi wamekuwa wakizitaka kwa ajili ya uchagunguzi chini ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Makosa ya Mitandao na kushindwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kuharibu uchunguzi chini ya kifungu cha namba 22 cha Sheria ya Makosa ya Mitandao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokuwa zimetolewa na tovuti ya JamiiForums jana, walisema kuwa ‘server’ ya tovuti yao haipo nchini Tanzania wala barani Afrika lakini hawakutaja ni nchi gani ilipo.

Melo apelekwa rumande Keko hadi Jumatatu Disemba 19 mwaka huu baada ya kukosa mdhamini katika shtaka la tatu la kumiliki na kuendesha tovuti ambayo haijasajiliwa nchini.

No comments: