ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 7, 2016

Wateja 15,345 wafaidika na Mradi wa Umeme wa KIA

 Naibu Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) akikagua Chumba cha kuongozea Mitambo ya Umeme kwenye Kituo cha kupoozea  Umeme cha KIA mkoani Kilimanjaro.  Kulia ni Mhandisi Neema Rushema, Mhandisi Nishati kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
 Naibu Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (katikati) akikagua Mitambo ya Umeme kwenye Kituo cha kupoozea Umeme cha KIA mkoani Kilimanjaro.  Kushoto Mhandisi Neema Rushema, Mhandisi Nishati kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Baadhi ya mitambo ya Umeme katika Kituo cha Kupoozea Umeme cha KIA.

Na Teresia Mhagama
Imeelezwa kuwa zaidi ya wateja wa awali 15,345 wameunganishwa na huduma ya umeme baada ya kukamilika kwa mradi wa Kituo cha Kupoozea Umeme cha KIA mkoani Kilimanjaro.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Kituo hicho.

Dkt. Pallangyo alisema kuwa, mradi huo ulihusisha ujenzi wa Transfoma mbili zenye uwezo wa Megawati 20 kila moja (2x20MVA) pamoja na jengo la kuendeshea mitambo ambapo Kituo kinasambaza umeme kwa wateja kupitia njia 6 za msongo wa kilovoti 33.

“Niseme tu kuwa, mradi huu ni muhimu sana kwani kukamilika kwake kumeboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Wilaya ya Hai, migodi ya Mirerani na maeneo mengine ya mkoa wa Kilimanjaro na Arusha,” alisema Dkt. Pallangyo.

Aliongeza kuwa Kukamilika kwa kituo hicho kumeimarisha pia upatikanaji wa umeme katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Alisema kuwa, utekelezaji wa Mradi huo ulianza rasmi tarehe 22 Machi, 2010 na gharama za mradi ni Shilingi bilioni 15.3 sawa na Dola za Marekani milioni 7.08.

Mradi huo wa KIA umetekelezwa kupitia Mradi wa TEDAP ulio chini ya Wizara ya Nishati na Madini ambao unahusika na uboreshaji wa njia za usafirishaji, usambazaji na ujenzi wa vituo vya umeme katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha na Kilimanjaro. 

Mradi wa TEDAP unahusisha Ujenzi wa njia za kusafirishia umeme wa msongo wa kilovolti 132, ujenzi wa vituo vitano vya kupozea umeme jijini Dar es salaam pamoja na Kituo cha kupozea Umeme cha KIA.

Mradi pia unahusisha ujenzi wa vituo vipya 19 vya kusambaza umeme wa msongo wa kilovolti 33 pamoja na njia za usambazaji umeme kwa urefu wa kilomita 102.497 za msongo wa kilovolti 33 na kilomita 34.018 za msongo wa kilovolti 11 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.

No comments: