ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 13, 2017

Kitanda cha kamba chazalishia wajawazito

By Azory Gwanda, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kibiti. Wajawazito wanaokwenda kupata huduma katika zahanati ya Kijiji cha Mchinga wilayani hapa Mkoa wa Pwani, hujifungua kwenye kitanda cha kamba kutokana na kutokuwapo maalumu cha kuzalishia.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya zahanati hiyo, Hamisi Mbonde alisema tangu ifunguliwe zaidi ya miaka 10 iliyopita wajawazito wanaokwenda kujifungua hapo hutumia kitanda cha kamba.

Mbonde alisema licha ya kuwapo jitihada za muda mrefu za kuomba kwa viongozi mbalimbali wa Serikali wilayani Kibiti ili zahanati hiyo ipatiwe kitanda cha kujifungulia wajawazito hazijazaa matunda.

Alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya ndugu huwasafirisha wajawazito kwenda katika zahanati ya Nyamisati.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Dk Martin Mwandike alithibitisha zahanati hiyo kutokuwa na kitanda cha kuzalishia wjawazito kwa muda mrefu.

Alisema alilikuta tatizo hilo baada ya Wilaya ya Rufiji kugawanywa na kuzaliwa Wilaya ya Kibiti.

Hata hivyo, alisema uongozi wa wilaya kupitia Idara ya Afya umeagiza kitanda hicho kwa ajili ya zahanati hiyo.

“Tayari tumeagiza kitanda cha kuzalishia wajawazito kwa ajili ya zahanati hiyo, pamoja na vitanda vingine vitatu vya kuzalishia ili kuondoa tatizo hilo kwenye zahanati nyingine tatu ambazo nazo hazina,” alisema.

Alisema mzabuni aliyepewa kazi ya kununua vitanda hivyo atakapovikabidhi kwao, watavipeleka kwenye zahanati hizo ili kuondoa tatizo hilo.

Mbali na vitanda maalumu kwa ajili ya kujifungulia, wajawazito wanahitaji huduma za dharura ikiwamo ya damu salama ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Huduma nyingine ni ya upasuaji inapotokea mjamzito ameshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida.

No comments: