WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema Serikali imetoa sh. bilioni 2.4 kwa ajili ya kuboresha mradi
wa maji katika mji wa Makambako mkoani Njombe
Ametoa kauli hiyo siku ya Alhamisi, Januari 19, 2017 wakati akizungumza na wananchi katika uwanja
wa Polisi Makambako ulipofanyika mkutano wa hadhara akiwa katika ziara yake ya
kikazi mkoani Njombe.
Waziri Mkuu alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi za salama
katika umbali usiozidi mita 400 kama inavyosema sera ya maji.
Hata hivyo aliwataka
wananchi kutofanya shughuli za kijamii katika vyanzo vya maji ili kuvilinda.
Alisema Serikali inatumia fedha nyingi kutafuta maji kwa sababu vyanzo vingi zimekauka
kutokana na shughuli za kibinadamu.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alizungumzia suala la madai
ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha ukaguzi cha pamoja na soko
la kitamaifa katika eneo la Makambako aliahidi kuwa watalipwa.
“Fidia zenu mtalipwa
hivi katibuni baada ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha
taratibu za ulipaji,” alisema. Wananchi hao walilalamikia ucheleweshwaji wa
malipo ya fidia hizo kupitia katika mabango mbalimbali pamoja na mbunge wa
Njombe, Mheshimiwa Deo Sanga.
Serikali imeanzisha
eneo la Idofi lililoko Makambako kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa
pamoja wa magari ya mizigo ili kupunguza vikwazo vya kibiashara barabarani kwa
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kituo hicho kitakuwa
na vituo vidogo vya Polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Maliasili pamoja na vituo vya mizani.
Awali mbunge wa jimbo
la Njombe Mheshimiwa Sanga alisema moja ya changamoto inayowakabili wakazi wa
mji wa Makambako ni ucheleweshwaji wa malipo ya fidia kwa waliopisha ujenzi wa
kituo hicho hali inayosababisha baadhi yao kwenda kudai fidia hiyo kwake.
”Mheshimiwa Waziri
Mkuu leo na sisi wananchi wa Makambako tutapona. Baba Majaliwa hawa wananchi
wanadai fidia yao kwa muda mrefu na baadhi yao wamefikia hatua ya kuja kulala
nje ya nyumba yangu wakigoma kuondoka hadi niwape ufafanuzi wa malipo yao,”
alisema.
Mbali na kuwasilisha
changamoto hiyo mbunge huyo pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa
jitihada zake za kuboresha maendeleo ya wananchi hususan wakazi wa jimbo la
Njombe.
Kwa upande wake mkuu
wa mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka alisema Serikali imetenga sh.
bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la chuma lenye urefu wa mita 95
katika mto Ruhuhu.
Alisema mkataba wa
ujenzi wa nguzo za daraja tayari umesainiwa kati ya mkandarasi wa kampuni ya
M/s Lukolo na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama ya sh bilioni
6.17 na muda wa utekelezaji ni miezi 24.
Akizungumzia mapambano
dhidi ya ugonjwa wa ukimwi Bw. Ole Sendeka alisema mkoa unaendelea na kampeni
za upimaji, zilizowezesha watu kufahamu afya zao na kuchukua tahadhari ya jinsi
ya kujikinga na kuepuka maambukizi mapya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 20,
2017.
No comments:
Post a Comment