Kaimu Mkuu wa Idara ya Miradi ya Ujenzi kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi Injinia Wambura M. Wambura akiongea na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu jukumu la ukaguzi wa kiufundi au kitaalam wa miradi ya ujenzi nchini jijini Dar es Salaam leo.(Picha na Benjamin Sawe- Maelezo)
Kaimu Mkuu wa Idara ya Majengo kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi Injinia Kissamo Fredrick akiongea na wanahabari kuhusu mafanikio ya Baraza hilo katika utekelezaji wa jukumu la kufanya ukaguzi wa kiufundi jijini Dar es Salaam leo.
SERIKALI kupita Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) imefanya ukaguzi wa miradi mikubwa 163 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2 ikijumuisha Barabara, majengo, maji na viwanja vya ndege.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu wa Idara ya Uhandisi wa Baraza hilo Mhandisi Wambura M. Wambura alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ukaguzi huo.
Mhandisi Wambura amesema kuwa miradi yote iliyofanyiwa ukaguzi inatekelezwa chini ya ufadhili wa Serikali.
“Shughuli za kiukaguzi zilizofanyika ni pamoja na kufanya mapitio na tathmini ya michakato ya manunuzi, utekelezaji wa mikataba, utekelezaji wa miradi,ongezeko la gharama za miradi, pamoja na ubora wa kazi zilizofanyika,” alisisitiza Mhandisi Wambura.
Aliongeza kuwa lengo la kaguzi hizo ni kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inalingana na ubora wa miundombinu iliyojengwa katika eneo husika.
Aidha, Mhandisi Wambura amesema kuwa katika kipindi cha 2015/2016 baraza lilifanya ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya matengenezo ya barabara kwa halmashauri zote za Wilaya pamoja na TANROADS kwa Mikoa ya Mbeya,Songwe,Rukwa,Katavi,Kigoma, na Shinyanga ambapo miradi hiyo iliyotekelezwa kwa fedha za mfuko wa Barabara.
Miradi mingine iliyofanyiwa ukaguzi wa kiufundi mwaka 2011 ni 14 iliyohusu ujenzi wa vituo vya afya na 36 ya ujenzi wa zahanati 50 iliyotekelezwa kwenye Halmashauri za Wilaya 20.
Akizungumzia changamoto zilizobainika katika ukaguzi unaofanywa na Baraza hilo Wambura alibainisha kuwa ni kutozingatiwa kwa taratibu za kusimamia ubora wa kazi na maandalizi hafifu ya miradi katika hatua za mwanzo katika utengaji bajeti yakutosha,usanifu na ukadiriaji gharama za ujenzi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya majengo Bw. Kissamo Elias alitoa wito kwa wadau wa sekta hiyo kulitumia Baraza hilo kufanya kaguzi katika miradi wanayotekeleza ili kuongeza tija hali itakayochochea ukuaji wa sekta hiyo.
Baraza la Taifa la Ujenzi ni kitovu cha uratibu wa sekta ya ujenzi kwa taasisi zote zinazoshughulika na shughuli za ujenzi pamoja na wadau ili kuleta umoja,uwiano, na ushirikiano katika utendaji ndani ya sekta ya ujenzi,Baraza linaendelea kusimamia na kuongoza juhudi za kukuza na kuendeleza sekta ya ujenzi nchini.
Baraza la Taifa la Ujenzi ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge namba 20 ya mwaka 1979 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2008,baraza lipo chini ya Wizara ya ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment