Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bw. Mohamed Kiganja akizungumza na wadau, walimu na viongozi wa vyama vya michezo nchini wakati wa ufunguzi wa mkutano wenye lengo la kutoa mafunzo kwao kuhusu madhara ya matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni uliofanyika katika Ukumbi ulipo katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam leo Januari 13, 2017.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. Alex Nkenyenge akisisitiza jambo kwa wadau, walimu na viongozi wa vyama vya michezo nchini wakati wa ufunguzi wa mkutano wenye lengo la kutoa mafunzo kwao kuhusu madhara ya matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni uliofanyika katika Ukumbi ulipo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo Januari 13, 2017.
Baadhi ya wadau, walimu na viongozi wa vyama vya michezo nchini wakifuatilia watoa mada wakati wa mkutano wenye lengo la kutoa mafunzo kwao kuhusu madhara ya matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni uliofanyika katika Ukumbi ulipo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam leo Januari 13, 2017. Picha zote na Raymond Mushumbusi WHUSM
Na Raymond Mushumbusi WHUSM
Wanamichezo nchini wameshauriwa kuzingatia mkataba wa kimataifa wa dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni ili kuwezesha kuiendeleza sekta ya michezo kwa kutoa washindi wanaostahili katika mashindano mbalimbali.
Ushauri huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye katika risala iliyosomwa kwa niaba yake na katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa(BMT) Bw. Mohamed Kiganja katika ufunguzi wa mkutano wa wadau,walimu na viongozi wa vyama vya michezo wenye lengo la kujadiliana kuhusu Mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.
Bw. Mohamed Kiganja ameongeza kuwa ili kufanikisha maendeleo ya michezo nchini yako mambo muhimu ya kuzingatia kudhibiti na kuzuia matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni utoaji wa elimu kwa wanamichezo kuhusu madhara ya utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu michezoni sanjari na utoaji wa adhabu kali kwa watakaobainika kutumia dawa au mbinu za kuongeza nguvu michezoni.
“Ushindi wowote unaopatikana baada ya mchezaji kutumia dawa ama mbinu nyingine yoyote chafu mbali ya kutokuwa haramu lakini pia inamyima ushindi yule mchezaji ambaye hatumii dawa na inapelekea kutokuwepo kwa ushindani wa kweli katika mashindano” alisistiza Bw. Kiganja.
Aidha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Moshi Kimizi amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kutoa mafunzo kwa viongozi wa michezo ambapo itasaidia kuipeleka elimu hiyo kwa wanamichezo walio chini ya vyama vyao.
Pia ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuendelea kushirikiana na wadau ili kupata Sheria itakayoendana na mkataba huo wa kimataifa ili kuiendeleza sekta ya michezo kwa manufaa ya wanamichezo na taifa kwa ujumla.
“Niiombe Serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya michezo kuendelea kushirikiana na wadau wa michezo na wanamichezo kudhibiti matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni ili kulinda heshima ya michezo na taifa kwa ujumla” Alisisitiza Dkt Kimizi.
Mkutano huo ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Habari utamaduni Sanaa na Michezo wenye lengo la kutoa mafunzo ya siku moja kwa wadau, walimu na viongozi wa vyama vya michezo nchini kuhusu madhara ya matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni umehusisha takriban washiriki 100 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment