ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 12, 2017

Talaka Ya Flora Mbasha Yagonga Mwamba Kortini

DAR ES SALAAM: Mwanamuziki nyota wa nyimbo za Injili, Flora Henry Mayala aliyefahamika awali kama Flora Mbasha, amegonga mwamba katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni baada ya kesi yake aliyoifungua ya kudai talaka kutoka kwa mzazi mwenziye ambaye pia ni mwana-gospo, Emmanuel Mbasha kugonga mwamba na kufutwa.
Katika kesi hiyo ambayo ni ya pili baada ya awali pia kutupwa nje, Flora alikuwa amefungua madai namba 119 ya mwaka 2016 ya kuomba talaka kwa mara ya pili lakini kwa sababu ya mahakama kukosa mamlaka ya kisheria kusikiliza madai hayo, iliamriwa kufutwa.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, wakili wa Flora, Boniphace Mahela alisema lengo la mteja wao lilikuwa ni kudai talaka na kugawana mali, lakini kutokana na sheria za kimahakama na pia upande wa pili wa mawakili wa Emmanuel kuweka pingamizi na wao kukosa vithibitisho vyote, wameamua kufuta kesi.

“Flora na Emmanuel walikuwa wakiishi Tabata na hiyo ipo katika Wilaya ya Ilala kwa maana hiyo kitu ambacho mahakama imekikataa ni kuileta kesi hii Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni. Pili tumeamua kuifuta kutokana na kutokidhi vithibitisho ambapo tumeamua tuifanye nje ya Mahakama, iwe kifamilia zaidi,” alisema Mahela.
Naye wakili wa Emmanuel, Ngassa Ganja alisema kuwa, baada ya kusikia madai hayo, waliamua kuweka hoja sita za pingamizi la awali ambapo limefanikiwa baada ya mawakili wa Flora kusikiliza.
“Mwaka 2014 Flora alipeleka madai ya talaka katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala namba 64. Madai hayo yalikuwa kudai talaka na mambo mengine ambapo kesi ilidumu kwa miaka miwili lakini aliamua kuifuta kwa sababu alizoona anaweza kutumia njia nyingine za kifamilia zaidi.
“Kabla ya mawakili wa Flora kuamua kuifuta kesi hii, tulikuwa tumeweka pingamizi tofauti kama sita. La kwanza, sheria ya ndoa ya mwaka 71 inataka unapoleta madai ya talaka ujue kwanza huko nyuma kama mlishawahi kupelekana mahakamani juu ya ndoa.
“Pili katika madai ya talaka ni lazima kuambatanisha hati ya usuluhishi wa ndoa kutoka sehemu husika ambapo wao walikuwa nayo ya Ustawi wa Jamii lakini inatakiwa isizidi miezi sita sasa wao walikuwa nayo ya zaidi ya miaka karibia mitatu. Sasa hivyo ndiyo vimewafanya kufuta kesi hii,” alisema Ngassa.
Emmanuel na mkewe Flora walipamba katika vyombo vya habari miaka michache iliyopita baada ya kuibuka mgogoro mkubwa katika ndoa yao, uliosababisha mwanaume kushtakiwa kwa madai ya kumbaka mdogo wa mke wake, kesi ambayo hata hivyo ilimalizika kwa mtuhumiwa kutokuwa na hatia.
Kwa sasa wawili hao kila mmoja yupo kivyake na mwimbaji huyo wa kike akitaka mashabiki wake wamtambue kama Madame Flora huku mume akitaka jina lake lisitumiwe tena na mkewe huyo wa zamani kwa namna yoyote.
GPL

No comments: