ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 18, 2017

MANJI ALAZWA TENA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

Baada  ya kupata dhamana ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, amelazwa tena kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Ofisa Uhusiano wa Taasisi hiyo jana, Anna Nkinda, Manji alifikishwa hospitalini hapo juzi jioni ikiwa ni muda mfupi baada ya kupata dhamana dhidi ya kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin inayomkabili.

“Ni kweli Manji yupo hapa, aliletwa jana jioni (juzi) kwa matibabu ambapo hadi leo (jana) ninavyoongea na wewe bado yupo hapa amelazwa anaendelea na matibabu kama kawaida,” alisema Anna.

Hii ni mara ya pili kwa Manji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, kulazwa kwenye taasisi hiyo.

Mara ya kwanza ilikuwa ni Februari 12, mwaka huu alipolazwa hapo akitokea katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alipokuwa ameshikiliwa tangu Februari tisa akifanyiwa mahojiano.


Mfanyabiashara huyo alifika mwenyewe kwenye kituo hicho cha polisi kutokana na wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyetaja majina 65 ya watu aliodai wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mbali na Manji, baadhi ya watu wengine waliotajwa na Makonda na kutakiwa kufika kituoni hapo ni Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan ambao tayari wamehojiwa polisi huku Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, akiwa bado hajahojiwa licha ya kutajwa kwenye orodha hiyo.

Juzi Alhamisi, Manji alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo shauri lake lilisikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha.

Karani wa mahakama hiyo, Sarah Mulokozi, alimsomea mshtakiwa shtaka lake ambapo alidai kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga Sea View jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Mtuhumiwa huyo alikana shtaka hilo na Mkurugenzi wa Mashtaka Msaidizi (ADPP), Osward Tibabyekomya, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Upande wa mawakili wa utetezi ambao ni Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo, waliiomba Mahakama kumpa mshtakiwa dhamana  kwa sababu ya mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.

Hakimu Mkeha alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kutakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10 pamoja na mdhamini mmoja wa kuaminika ambapo Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Mkwasa, alimdhamini Manji, ambaye aliachiwa kwa dhamana hadi Machi 16.

Mara baada ya kupata dhamana, Manji aliondoka mahakamani hapo saa 9:40 akiwa kwenye gari yenye namba T670 BBX aina ya Hummer.

No comments: