Wakati Serikali ikiendelea kujipanga kwa vita dhidi ya dawa za kulevya, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kutotangaza majina ya watuhumiwa kabla ya kufanyika uchunguzi na kujiridhisha.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kulaumiwa na watu tofauti kwa kitendo chake cha kutangaza majina ya watu aliotaka kufanya nao mahojiano kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Wengi waliokosoa kitendo hicho, hasa wabunge, walisema kutangaza majina ni kuharibu uchunguzi na pia kunachafua watu kabla ya kuthibitika kuwa wanajihusisha na dawa hizo na kwamba chombo pekee kinachoweza kumtia mtu hatiani ni mahakama.
Watu walioitwa kituo cha polisi jijini Dar es Salaam, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa, viongozi wa dini na wasanii walihojiwa na baadhi kupekuliwa majumbani na ofisini kwao kabla ya kwenda kupimwa.
Baadhi ya watuhumiwa hao ni kiongozi wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji na msanii nyota wa filamu, Wema Sepetu.
Akizindua Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya uliofanyika ofisi ya waziri Mkuu jana, Majaliwa alisema wakuu wa mikoa wana nafasi nzuri ya kushiriki katika vita hiyo kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu.
“Wakuu wa mikoa mna kazi kubwa katika vita hii. Mkiwa wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama, mpo kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema Waziri Mkuu mbele ya mawaziri ambao ni wajumbe wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya na wakuu wa mikoa.
“Jiepusheni kuwatangaza watuhumiwa kabla hatujafanya uchunguzi. Itakapotokea uchunguzi umekamilika na kuwakamata watuhumiwa, msisite kuwatangaza kwenye vyombo vya habari, msiogope. Serikali inawategemea na itaendelea kuwaunga mkono,” alisema.
Pamoja na hayo, Majaliwa alisema Serikali haitawavumilia watendaji wa mamlaka watakaochukua rushwa kwa lengo la kuwasaidia wahusika wa dawa za kulevya.
Alisema anafahamu kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni vita kubwa na hilo linatokana na kuhusisha wafanyabiashara wakubwa na watu maarufu.
“Watendaji wa mamlaka kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kufahamu kuwa mmeaminiwa, hivyo muwe waadilifu kwani mmekabidhiwa makubwa yanayohitaji uangalifu wa hali ya juu,” alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya udhibiti wa dawa hizo nchini na hilo litafanyika bila uonevu wala upendeleo.
“Dawa za kulevya ni tatizo kubwa. Tanzania imekuwa ikitumika kama njia ya kupitishia dawa hizo, hivyo mapambano yanapaswa kufanyika kwa nguvu kubwa. Sheria ya udhibiti isimamiwe kikamilifu; masharti yote yaliyotajwa yatekelezwe bila kumuonea mtu,” alisema Majaliwa ambaye kwa nafasi yake anakuwa mwenyekiti wa baraza hilo.
Alisema baraza hilo lina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera ya udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
“Jukumu hili ni kubwa. Sisi kama wajumbe wa baraza tunatakiwa kulitekeleza kwa uadilifu na umahiri mkubwa. Sina shaka na wajumbe,” alisema.
No comments:
Post a Comment