Marufuku hiyo ilipiga marufuku wahamiaji na wageni kutoka nchi hizo saba - Iran, Iraq, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen - kuingia Marekani, lakini utekelezaji wake ulisitishwa na mahakama wiki iliyopita.
Jopo la majaji watatu limeuliza maswali kuhusu upeo na kikomo cha madaraka ya rais na ushahidi ambao Bw Trump alitumia kufanya uamuzi huo.
Aidha, majaji hao wameuliza maswali kuhusu iwapo hatua hiyo inafaa kuchukuliwa kuwa ubaguzi.
Uamuzi wa majaji hao unatarajiwa baadaye wiki hii.
Bila kujali uamuzi wa mahakama hiyo, iwapo itaunga mkono au kupinga amri hiyo ya Bw Trump, kuna kila dalili kwamba kesi hiyo itapelekwa Mahakama ya Juu.
Kulikuwa na kipindi cha kila upande kueleza na kufafanua msimamo wao Jumanne.
Wizara ya haki (serikali) ilikuwa ya kwanza kujitetea, ambapo mawakili wake waliwahimiza majaji kurejesha marufuku hiyo.
Wakili August Flentje alisema Bunge la Congress liliidhinisha rais kuamua na usemi kuhusu nani anaweza kuingia nchini Marekani.
ALipotakiwa kueleza ushahidi kwamba mataifa saba ambayo yameathiriwa ni tishio kwa Marekani, alisema kuna Wasomali kadha Marekani ambao wana uhusiano na kundi la kigaidi la al-Shabab.
Wakili anayewakilisha jimbo la Washington alisema hatua ya mahakama kuzima marufuku hiyo haikuwa imeathiri serikali ya Marekani kwa vyovyote vile.
Mwanasheria mkuu wa jimbo hilo Noah Purcell alisema marufuku hiyo ilikuwa imeathiri maelfu ya wakazi wa jimbo hilo. Alisema wanafunzi wengi walicheleweshwa wakijaribu kufika Washington na wengine walikuwa wamezuiwa kutembelea jamaa zao wanaoishi nje ya nchi hiyo.
Ni marufuku dhidi ya Waislamu?
Dakika za mwisho za kikao hicho ziliangazia kuhusu iwapo marufuku hiyo ya usafiri ni sawa na kuwazuia Waislamu kuingia Marekani, jambo ambalo lingekuwa kinyume cha katiba.
Taarifa ya kurasa 15 iliyotolewa na Wizara ya Haki Jumatatu usiku ilisema agizo hilo la rais "haliegemei upande wowote kuhusiana na dini".
Mahakamani, Jaji Richard Clifton alitaka pande zote mbili kueleza iwapo kuna thibitisho kwamba marufuku hiyo ilikusudiwa kuwabagua Waislamu, na kutaja kwamba marufuku hiyo itaathiri tu asilimia 15 ya Waislamu duniani.
Bw Purcell aligusia matamshi ya Bw Trump wakati wa kampeni alipozungumzia kuwapiga marufuku Waislamu wasiingie Marekani kwa muda.
Aidha, alirejelea pia tamko lililotolewa na mmoja wa washauri wa rais, Rudy Giuliani, aliyesema alitakiwa kuunda njia ya kuhakikisha marufuku dhidi ya Waislamu inatekelezwa kwa njia isiyovunja sheria.
Bw Clifton pia alisema nchi saba zilizowekewa marufuku zilitambuliwa na utawala wa Obama na Bunge la Congress kuwa nchi zilizohitaji masharti makali zaidi ya viza, kutokana na tisho la ugaidi.
Aliuliza: "Unakubali kwamba uamuzi wa utawala uliopita na Bunge la Congress pia uliongozwa na dini?"
La hasha, Bw Purcell alijibu, lakini Rais Trump ameitisha marufuku kamili na ingawa hii ya sasa si marufuku kamili, ni ubaguzi.
ipengee muhimu vinasema:
raia wa nchi za Iraq, Syria, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen - hata wenye viza - ni marufuku kuingia Marekani;
marufuku ya muda kwa wakimbizi wote;
kupewa tena kipaumbele kwa msingi wa dini (kwa maana ya Ukristo) katika kuwapa wakimbizi hifadhi;
marufuku kwa wakimbizi wote wa Syria;
kuweka kipimo kwenye jumla ya wakimbizi wanaoingia Marekani kila mwaka kuwa 50,000.
BBC
No comments:
Post a Comment