ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 8, 2017

alada la kesi dhidi ya ‘Mpemba’ kuhamishiwa mahakama ya mafisadi




Dar es Salaam. Jalada la kesi ya kujihusisha na mtandao wa kihalifu na kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh785 milioni inayomkabili Yusuf Ali Yusuf ‘Mpemba’ aliyetajwa na Rais John Magufuli ipo kwenye maandalizi ya kuhamishiwa Mahakama ya Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Kwa mujibu wa utaratibu, kesi hiyo itahamishiwa Mahakama ya Mafisadi iwapo vijalada vyenye kumbukumbu za mashahidi wa upande wa upelelezi na upande wa mashtaka, vitakuwa vimekamilika.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Elia Athanas alitoa angalizo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba kwamba ni muhimu akaweka kumbukumbu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Maelezo hayo yalipata nguvu kutoka kwa wakili wa upande wa utetezi, Nehemiah Nkoko ambaye aliutaka upande wa mashtaka wamshinikize Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) avikamilishe vijalada hivyo haraka ili kesi iende Mahakama ya Mafisadi.

Hakimu Simba aliwaambia upande wa mashtaka kuwa anachofahamu utaratibu unaofuata baada ya jalada kuwa kwa RCO ni lazima liende ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na baadaye washtakiwa wasomewe vijalada hivyo ambavyo vinahusisha maelezo ya mashahidi na vielelezo kabla ya kuhamishiwa Mahakama ya Mafisadi.
Mwananchi

No comments: