ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 9, 2017

Mshirika wa Osama Bin Laden auawa na wanajeshi wa Marekani Syria

Ndege ya kivita ya Marekani
Wanajeshi wa Marekani wanasema wamewaua wanachama 11 wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda kupitia mashambulio mawili ya kutoka angani karibu na mji wa Idlib nchini Syria mwezi huu.

Miongoni mwa waliouawa ni mshirika mkuu wa zamani wa aliyekuwa kkiongozi wa al-Qaeda Osama Bin Laden, wizara ya ulinzi ya Marekani imesema.

Kapteni Jeff Davis, ambaye ni msemaji katika wizara hiyo, amesema wanachama 10 waliuawa kwenye shambulio moja Februari 3.

Shambulio la pili tarehe 4 Februari lilimuua Abu Hani al-Masri, aliyekuwa na ushirika wa karibu sana na Osama Bin Laden.

Al-Masri adnadaiwa kuanzisha na kuendesha kambi za mafunzo za al-Qaeda nchini Afghanistan miaka ya 1980 na 1990.

Kadhalika, alikuwa pia na uhusiano wa karibu na Ayman al-Zawahiri, ambaye alichukua uongozi wa al-Qaeda when Bin Laden alipouawa na wanajeshi wa Marekani 2011.

"Mashambulio haya yanavuruga uwezo wa al-Qaeda kupanga na kutekeleza mashambulio ya moja kwa moja ya kulenga Marekani na maslahi yake kote duniani," amesema Kapteni Davis.

Al-Qaeda kwa sasa sana huendesha shughuli zake Syria kupitia kundi la kijihadi la Jabhat Fateh al-Sham ambalo awali lilifahamika kama al-Nusra Front.

Kundi hilo lilitangaza katikati mwa mwaka 2016 kwamba halikuwa tena na uhusiano na makundi ya nje, na kuashiria kwamba huenda lilivunja uhusiano na al-Qaeda ingawa halikutaja kundi hilo moja kwa moja.

Inaaminika kwamba uongozi wa Fateh al-Sham bado una uhusiano na al-Qaeda.

Shambulio la Marekani dhidi ya wanachama wa al-Qaeda nchini Yemen wiki iliyopita, operesheni ya kwanza ya kijeshi kuamrishwa na Donald Trump, ilisababisha kifo cha mwanajeshi mmoja na vifo vya raia 16 wakiwemo watoto, taarifa zinasema.

Utawala wa Trump hata hivyo ulisema operesheni hiyo ilifanikiwa na imeiwezesha Marekani kupata habari nyingi za kijasusi.

BBC

No comments: