Baadhi ya Watanzania waliofukuzwa Msumbiji wakitoka ofisi ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Avod Mmanda jana. Picha na Haika KimaroBy Haika Kimaro,
Mtwara. Mmoja kati ya Watanzania 180 waliokuwa wakiishi nchini Msumbuji na kudaiwa kufanyiwa ukatili amesema alibakwa na askari watatu kabla ya kuwekwa mahabusu.
Kauli ya mwanamke huyo (jina tunalihifadhi) imekuja wakati Serikali ikiahidi kufanya uchunguzi wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika kutimua Watanzania nchini Msumbiji.
Akisimulia mkasa huo, amesema walianza kufukuzwa usiku Februari 11, muda ambao askari hao waliutumia kumfanyia kitendo hicho.
Amesema alisikia watu wakivunja geti la nyumba waliokuwa wakiishi na kudhania ni majambazi, kumbe ni askari ambao waliwalazimisha kutoa nyaraka zao zote za kuishi Msumbiji pamoja na pesa.
“Nilimwambia mume wangu watakuwa ni majambazi, akajificha chini ya uvungu, lakini wakamtoa na baadaye kututoa ndani na kuanza kutupiga,” amesema.
Amesema walilazimishwa kutoa mali zao ndani na zikawekwa kwenye gari la polisi na kisha kuwafunga mikono na baadaye kuwapeleka mahabusu.
Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Mtwara, Rose Mhagama amesema idadi ya Watanzania waliorudi na kusajiliwa katika mpaka wa Kilambo ni watu 221 hadi kufikia jana mchana.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo kilichopo mpakani na Msumbiji, Mohamed Mkama alisema wananchi wa kijiji chake wamekuwa wakishirikiana na wanakijiji wa vijiji jirani vya Msumbiji, lakini tukio hilo limewashangaza.
Amesema wamekuwa wakitembeleana na hata wengine kutoka upande wa Msumbiji kuja kutibiwa Tanzania kutokana na ujirani mwema.
No comments:
Post a Comment