TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Naibu Katibu Mkuu awatembelea Watanzania wanaoshikiliwa nchini Malawi
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi jana aliwatambelea Watanzania wanane wanaoshikiliwa katika Gereza Kuu la Mzuzu nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kinyume cha sheria katika mgodi wa urani wa Kayerekera.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu alifuatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Hassan Bendeyeko pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi,aliwasihi watu hao kuwa wavumilivu wakati Serikali ikitafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Balozi Mwinyi aliwaeleza Watanzania hao kuwa mazungumzo katika ngazi mbalimbali kati ya Tanzania na Malawi yanaendelea na kuna matumaini makubwa kuwa hivi karibuni ufumbuzi wa suala lao unaweza kupatikana.
Balozi Mwinyi aliendekea kuekeza kuwa yeye na wenzake wamekuja Lilongwe kushiriki kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi, lakini wameamua kusafari takriban kilomita 400 kutoka Lilongwe hadi Mzuzu kuja kuwaona na kuwafikishia ujumbe kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha kuwa suala hili linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
"Nikufahamisheni kuwa jitihada katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo lenu zinaendelea na hata Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokutana na Rais wa Malawi, Mhe. Prof. Peter Mutharika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia jambo lenu lilikuwa moja ya masuala waliyoyajadili.
Naibu Katibu Mkuu alisema kuwa alifarijika kuwakuta watu hao wote wapo salama na wenye afya nzuri na kuwajulisha kuwa ziara hiyo ya kuwatembelea na nyingine zilizofanyika siku za nyuma ni ushahidi dhahiri kwao na kwa Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. Magufuli imedhamiria kuwahudumia Watanzania wote wa kada mbalimbali popote pale wanapoishi.
Watanzania hao wanane walikamatwa mwishoni mwa mwezi Desemba, 2016 na hadi sasa wanashikiliwa katika gereza kuu la Mzuzu. Watanzania hao ambao kati yao wawili ni wanawake wamejitambulisha ni wakulima na wachimbaji wadogo wa madini wanatoka katika mkoa wa Ruvuma na walikwenda Malawi chini ya Taasisi ya CARiTAS kujifunza athari za migodi ya urani katika jamii.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Tarehe 05 Februari 2017
No comments:
Post a Comment