Wednesday, February 15, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

JAMHURI YA MUUNGANO TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA
MASHARIKI





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Taarifa kuhusu Watanzania waliopata matatizo nchini Msumbiji

Tumepokea taarifa za kukamatwa na kufukuzwa kwa raia wa Tanzania waliokuwa wakiishi katika mji wa Monte Puez ulio Cabo Delgado, Jamhuri ya Msumbiji.

Serikali ya Msumbiji imekiri kuwepo kwa operesheni maalum ya kuwakamata na kuwarudisha raia wa nchi za kigeni wanaoishi katika mji huo bila kufuata Sheria za Uhamiaji za nchi hiyo. Aidha, Serikali hiyo imetaarifu kwamba, zoezi hilo limeanzia mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa kigeni ikilinganishwa na miji mingine.

Kufuatia hali hiyo, Ubalozi weti nchini Msumbiji upo eneo la tukio ili kufuatilia suala hili na kujionea hali halisi. Aidha, unaendelea kufanya mawasiliano ya Kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao. Inakadiriwa kuwa, Watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji huo wa Monte Puez.


Kuanzia zoezi hilo lilipoanza, Raia wa Tanzania wapatao 132 wamesharudishwa nchini. Tarehe 11/02/2017 walirejeshwa raia 58. Tarehe 14/02/2017 wamerejeshwa raia 24 na leo tarehe 15/02/2017 wamesharejeshwa raia 50.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia Watanzania kuwa uhusiano kati ya Tanzania na jirani yetu Msumbiji ni mzuri. Hivi karibuni mwezi wa Desemba 2016, Tanzania na Msumbiji zilifanya mkutano wa ujirani mwema uliolenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Mkutano huo uliofanyika kwenye mji wa Pemba ulio Cabo Delgado uliainisha maeneo ya ushirikiano yakiwemo masuala ya biashara na uhamiaji.

Serikali inaendelea kuwakumbusha Watanzania wote waishio ughaibuni, kufuata Sheria na taratibu za nchi hizo wanazoishi.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
DAR ES SALAAM. 15 Februari, 2017.

1 comment:

Anonymous said...

WAsisahau tulivyowakomboa na kuwatoa kwenye ukoroni wa Mreno. Watanzania tulimwaga sana damu yetu. Inabidi wakumbushwe jinsi tuliyowatunza mamilioni ya wakimbizi wa Msumbiji. Nadhani Samora Machel angekuwa bado hai, angefedheheka kuona Msumbiji ya 2017 inafanya jambo hili. Wametulipa nini kwa mema mengi tuliyowafanyia?