ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 1, 2017

Uhakiki TIN wapasua kichwa

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa
By Kalunde Jamal, Mwananchi kjamal@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ikiwa jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho wa uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) mkoani Dar es Salaam, vituo vingi vilikuwa na misururu ya watu huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikisisitiza haitaongeza muda.

TRA ilipanga kuhakiki na kuboresha taarifa za TIN kwa siku 60, kuanzia Agosti hadi Oktoba 2016 lakini kutokana na wingi wa watu iliongeza hadi Novemba 30, hata hivyo iliongeza kwa mara ya tatu hadi jana, Januari 31.

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jana kwamba hawataongeza muda na jana ilikuwa ni siku ya mwisho.

“Lazima hatua nyingine zifuate, hatutaongeza muda kwa Dar es Salaam tutakuwa tumemaliza na tusonga mbele,” alisema.

Hata hivyo, watu waliojitokeza kuhakiki TIN zao walikuwa na maoni tofauti kuhusu suala hilo, Hamisi Kidanto aliyekuwa katika Kituo cha Millenium Tower kilichopo Kijitonyama Wilaya ya Kinondoni, aliuita utaratibu huo kama kumkomoa na kumsumbua mlipakodi anayelipa kwa hiari.

Alisema haamini kama kufanya hivyo ndiyo njia pekee ya kuhakiki taarifa za mlipakodi.

“Wanatukomoa, asubuhi nimekwenda Kituo cha Uwanja wa Taifa ambako niliambiwa hakuna foleni, nilichokuta anajua Mungu, nikaja hapa nusura nipoteze mwelekeo na kurudi nyumbani.

“Nina saa ya nne sielewi naelekea wapi na kufanya zaidi ya kununua fomu Sh500 hapo kwenye duka linalouza vifaa vya ofisini na kujaza,” alisema Kidanto.

Katika kituo cha Ilala, hali ilikuwa tofauti kidogo baada ya kuwapo utaratibu wa kukusanya fomu zilizojazwa kisha kuita mtu mmoja mmoja na kwa ajili ya hatua inayofuata.

Janeth Mathias aliyekutwa kwenye kituo hicho, alisema utaratibu huo ni mzuri lakini watu ni wengi, hivyo kuna kila dalili itafika saa kumi na moja jioni ya jana wakiwa bado wapo kituoni hapo.

No comments: