ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 23, 2017

WACHIMBAJI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA KUEPUSHA AJALI MIGODINI

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wachimbaji wadogo kwenye machimbo ya dhahabu ya Musasa yaliyopo kwenye Kata ya Makurugusi, Wilayani Chato. Nyuma yake ni baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini.
 Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini kwenye machimbo ya dhahabu ya Musasa katika Kata ya Makurugusi, Wilaya ya Chato wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani).
 Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini kwenye machimbo ya dhahabu ya Musasa katika Kata ya Makurugusi, Wilaya ya Chato wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani).
Muonekano wa baadhi ya maeneo ya machimbo ya dhahabu ya Musasa katika Kata ya Makurugusi, Wilaya ya Chato.

Wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kufanya shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama migodini ili kuepusha ajali.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu kwenye mgodi wa Musasa uliopo Kata ya Makurugusi, wilayani Chato.
Dkt. Kalemani alisema njia bora ya kuepukana na ajali migodini ni kufanya shughuli za uchimbaji kwa kutii sheria za uchimbaji madini bila shuruti na kuzingatia kanuni za usalama kwenye maeneo ya machimbo na wakati wa shughuli za uchimbaji.
Aliwaasa wachimbaji wadogo wa madini kote nchini kujifunza kutokana na ajali mbalimbali zilizotokea migodini ili kuepuka sababu zilizopelekea kutokea kwa ajali hizo kutojirudia tena kwenye maeneo mengine.
Aidha, Dkt. Kalemani aliwasisitiza wachimbaji wa madini kote nchini kuhakikisha wanafanya shughuli za uchimbaji kwa kutunza mazingira na afya zao pamoja na afya za wengine wanaozunguka machimbo husika.
Alisema suala la mazingira linapaswa kupewa kipaumbele wakati wa shughuli husika, na kwamba ni jukumu la kila mchimbaji na kila anayeishi ama kufanyia shughuli zake maeneo ya machimbo kuhakikisha anaboresha mazingira ili kuepusha majanga mbalimbali ikiwemo ya magonjwa ya mlipuko.
“Chimbeni madini kwa kutunza mazingira na afya zenu ili mpate kufaidi matunda yatokanayo na shughuli hii, alisema Dkt. Kalemani.
Kwa wakati huohuo, Naibu waziri huyo aliwakumbusha wachimbaji wadogo wa madini kulipa kodi na ushuru stahiki ili kuepuka usumbufu.
Aliwahakikishia wachimbaji wadogo wa madini kufanya shughuli zao bila kubughudhiwa endapo watafuata maelekezo ya sheria.
“Mkitaka kuishi salama na kufanya shughuli zenu bila kubughudhiwa, hakikisheni mnalipa kodi na tozo mbalimbali mnazopaswa kulipa,” alisema.
Dkt. Kalemani alizipongeza kampuni za watanzania zinazomiliki leseni kwenye machimbo hayo ya Musasa ambazo ni Godfrey and Partners, Kilimo Kwanza Group na Hapa Kazi Tu Group kwa kuonesha njia na kutunza usalama kwenye machimbo hayo na hivyo kuwataka wachimbaji wengine kuiga mfano huo.

No comments: