ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 3, 2017

Wafanyabiashara wa Tanzania tupo tayari kwa ubia- Dkt Mengi

 Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi (katikati) akifurahi jambo na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) Dr. Samwel Nyantahe (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye hafla ya chakula cha mchana na kuwapongeza mabalozi wapya wa Tanzania nje ya nchi iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye akiwasilisha 'presentation' iliyoainisha maeneo muhimu ya fursa za kibiashara kwenye masoko ya kimataifa kwa mabalozi wapya wa Tanzania nje ya nchi walioapishwa hivi karibuni wakati wa hafla ya chakula cha mchana kwa mabalozi hao iliyoandaliwa na TPSF jijini Dar es Salaam
  Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akizungumza na mabalozi wapa wa Tanzania nje ya nchi kwenye hafla ya chakula cha mchana na kuwapongeza mabalozi hao watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Italy, China, UN Geneva na Brazil iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akisisitiza jambo kwa mabalozi wapya watakaoiwakilisha Tanzania kwenye nchi za Uturuki, Italy, China, Brazil na UN Geneva (hawapo pichani) katika hafla ya chakula cha mchana na kuwapongeza mabalozi hao iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini–CTI Dr. Samwel Nyantahe akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika uwekezaji, kutafuta masoko mapya, kubadilishana bidhaa na utafutaji fursa za biashara kwenye masoko ya kimataifa kwa wafanyabiashara katika hafla ya chakula cha mchana na kuwapongeza mabalozi wapya watakaoiwakilisha Tanzania kwenye nchi za Uturuki, Italy, China, Brazil na UN Geneva iliyoandaliwa na TPSF katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam
 Mwenyekiti wa Tanzania Saccos For Women Entrepreneurs (TASWE - SACCOSS), Anna Matinde akizungumzia umuhimu wa kumshirikisha mwanamke katika ukuzaji wa biashara kubwa na ndogo ndogo, ambapo amesema wanawake ni nguzo muhimu katika ukuaji wa sekta binafsi nchini kutokana na uchapaji kazi wao katika sekta mbalimbali.
 Balozi mpya wa Tanzania nchini Uturuki, Prof Elizabeth Kiondo  akitoa shukrani kwa TPSF kwa kuandaa hafla fupi kama hiyo ya kubadilishana mawazo kwa jinsi gani wanaweza kukuza diplomasia ya kiuchumi katika vituo vyao vya kazi walipopangiwa.
 Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, akizungumza kwenye hafla hiyo  ambapo amesisitiza wafanyabiashara kutoka Tanzania watumie fursa adimu ambayo ipo kati ya Tanzania na China ambapo mahusiano na ushirikiano ulianza tangu enzi za Mao na Mwalimu Nyerere.
 Balozi wa Tanzania, Geneva, Dkt. James Msekela akisisitiza jambo kwa bodi ya TPSF kwenye hafla ya chakula cha mchana kwa mabalozi hao wapya iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Wafanyabiashara wa Tanzania wamesema wapo tayari kwa kufanya ushirikiano wa kibiashara wa ubia na wafanyabiashara kutoka nje ili kukuza diplomasia ya kiuchumi na mataifa mengine.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha mchana na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichoandaliwa na Taasisi ya sekta binafsi (TPSF) nchini, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Dkt. Reginald Mengi amesema wafanyabiashara watanzania si omba omba na wapo tayari kwa kufanya biashara ya ubia na wenzao.

“Napenda kusisitiza kwamba sisi watanzania si omba omba kwa wafanyabishara wa nje, tuna nia uwezo, ujuzi na tunajiamini kwa kufanya biashara za kimataifa kwa ubia ili kukuza uchumi wa nchini zetu,” amesema Dkt. Mengi.

Amesema kwamba fursa za uwekezaji zipo nchini kwenye sekta za kilimo, mafuta, gesi, usindikaji na mawasiliano ila ni muhimu kuunganisha nguvu za wafanyabiashara ili kuweza kupata matokeo chanya.

Dkt. Mengi alilisisitiza kwamba sekta binafsi nchini ina imani kubwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika adhma yake ya kukuza sekta ya viwanda ili kutatua tatizo la ajira na kuongeza mapato ya nchini.

“Ni muhimu kuimarisha sekta binafsi ili iweze kutoa mchango mkubwa katika uanzishwaji wa viwanda hapa nchini, kwa vyovyote vile sekta hii binafsi ndio itakayojenga viwanda hapa Tanzania,” aliongeza

Kwa Upande wa Mabalozi, Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye anakwenda kuiwakilisha nchi huko Brazil, amesema kwamba mabalozi ni kiungo muhimu kati ya wananchi wa mataifa husika katika kukuza mahusiano na ushirikiano wa kimataifa.

“Sisi ni wawakilishi wenu huko kwenye mataifa ya nje na zaidi na kukuza mahusiano au diplomasia ya kiuchumi kwa maslahi ya wananchi wetu,” amesema Dkt. Nchimbi

Naye Balozi wa Tanzania, Geneva, Dkt. James Msekela amesema kwamba ni muhimu kuanzisha mawasiliano ya mara kwa mara kati ya wafanyabishara na mabalozi ili kusaidia upatikanaji wa taarifa za fursa mbalimbali za uwekezaji au masoko kutoka kwenye bidhaa za nyumbani.
“fursa zipo kwenye kila sekta ni muhimu wafanyabishara wa ndani wakajenga uaminifu na kujiamini ili kuweza kuingia katika ushindani wa kibiashara katika soko la kimataifa,” amesema Dkt. Msekela.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Geofrey Simbeye amesema wataanzisha mawasiliano ya kudumu na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi ili kuweza kubadilishana mawazo na taarifa juu ya fursa za kibiashara katika nchi wanazokwenda kuwakilisha.

Alifafanua kwamba serikali imefungua milango kwa sekta binafsi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kukuza uchumi wa Tanzania na kuondoa tatizo la umaskini.
Kikao hicho kati ya sekta binafsi na mabalozi wa Tanzania wanaokwenda kuwakilisha nchi katika mataifa matano ambapo mabalozi hao ni Dkt Emmanuel Nchimbi-Brazil, Dkt. James Msekela-Geneva, Profesa Elizabeth Kinyondo-Uturuki, Mbelwa Kairuki-China na Balozi George Madafa- Italy

No comments: