Wajawazito na watoto katika maeneo mengi ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wamekosa huduma za msingi za chanjo na ushauri mwingine wa kiafya, huku kina mama wajawazito wakijifungua njiani na kupata matatizo mbalimbali ya uzazi, kutokana na umbali mrefu wa kuvifikia vituo vya afya na zahanati zinazotoa huduma hiyo.
Maria Mayanda ni mkazi wa kitongoji cha Mikochini Namawala B, kata ya Namawala wilayani Kilombero, ambaye ni miongoni mwa kina mama waliojifungulia njiani, kutokana na umbali wa zaidi ya kilometa 40 kufikia zahanati au kituo cha afya, ambaye anadai kupata tatizo hilo baada ya mito ya maeneo yao kufurika maji nyakati za mvua na njia kushindwa kupitika kirahisi, hali iliyofanya viongozi wa maeneo hayo wakiongozwa na mwenyekiti wao matia nyambo,kuhamasishana na kujenga banda maalum kwaajili ya kupatiwa huduma za mkoba yaani mobile cliniki.
Shirika la Plan International Tanzania kwa msaada wa kampuni ya Dalichi Sankyo kutoka Japan, wameona changamoto hizo na kuanzisha mradi wa miaka mitatu wa huduma za mkoba, ili kuisaidia serikali kutokomeza maradhi yanayozuilika na kupunguza vifo vya watoto na akina mama wilayani Kilombero, kwa kuwezesha huduma za chanjo katika maeneo magumu kufikika na yaliyo mbali na vituo vya afya, nia hasa ikiwa kutokomeza magonjwa kama surua, polio, kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, kichomi, nimonia na pepopunda kwa watoto wa hadi miaka mitano kwa kutumia chanjo,
Mpango huo utakaofanywa bure, ukiwa unagharimu milioni 660 hadi kukamilika, umekwenda sambamba na halmashauri hiyo kukabidhiwa gari kwaajili ya huduma za mkoba zitakazotolewa kwa kata 18, ambapo Mkurugenzi wa halmashauri ya Kilombero Denis Londo, aliyeomba msaada zaidi wa pikipiki tano kurahisisha upelekaji huduma, amekiri mwaka jana wameshindwa kufikia lengo la kutoa chanjo kwa asilimi 95 kama wizara ya afya ilivyogiza badala yake wakatoa asilimia 85 tu lakini wanaimani hali hiyo itapungua kupitia mradi huo, huku mkuu wa wilaya ya kilombero james ihunyo,akibainisha dhamira ya serikali ya awamu ya tano kutokomeza vikwazo vinavyosababisha vifo kwa mama na mtoto kwa kukosa huduma.
Katika mwaka 2013, wilaya ya Kilombero ilikuwa na vifo 144 vitokanavyo na uzazi kwa kila vizazi hai 1,000 huku vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano vikiwa vinne kati ya vizazi hai 1,000, na hadi sasa wilaya hiyo ina vituo vichache vinavyotoa huduma ya chanjo, ambapo kati ya vituo vya afya 63, ni vituo 40 tu vinavyotoa huduma za mkoba na kupitia mradi huo Kilombero wameainisha vituo 66 vilivyo umbali wa zaidi ya kilometa 35 kutoka vituo vya afya ambavyo ni vigumu kufikika kirahisi lakini mradi huo utafikia vituo 49 tu.
CHANZO
: ITV TANZANIA
No comments:
Post a Comment