Askofu Gwajima alidai hayo wakati akitoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuhusu kesi yake ya kushindwa kuhifadhi silaha.
Mbali ya Gwajima anayekabiliwa kwa kosa hilo, washitakiwa wengine ni mfanyabiashara anayedaiwa kuwa mlinzi wake, George Mnzava, Msaidizi wake, Yekonia Bihagaze na Mchungaji George Milulu ambao wanakabiliwa na kosa la kumiliki silaha isiyokuwa yao.
Akiongozwa na wakili wake, Peter Kibatala, Gwajima alidai kuwa Machi 27, 2015 anakumbuka alikuwa safarini kuelekea Arusha kwenye kikao cha maaskofu, ambapo aliondoka jijini Dar es Salaam, Machi 26,2015.
Alieleza kuwa wakati alipokuwa njiani kuelekea Arusha aliona taarifa kwenye mtandao wa kijamii kuwa Askofu Gwajima anatafutwa na Jeshi la Polisi.
Alieleza kuwa alishangaa kuiona taarifa hivyo, hivyo akafika hadi Arusha, lakini alishindwa kushiriki katika mkutano huo badala yake alianza safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda kuripoti kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Kanda ya Dar es Salaam.
Askofu Gwajima alieleza kuwa alifika jijini Dar es Salaam saa 9:30 alasiri ambapo aliunganisha hadi kituoni hapo na kukutana na Ofisa Mpelelezi wa Kanda (ZCO).
Kibatala alipomuuliza alikuwa na nani katika safari hiyo, Gwajima alieleza kuwa aliambatana na msaidizi wake, Bihagaze ambapo alikutana na ZCO wa wakati huo, aliyemtambua kwa jina la Masawe.
Alieleza kuwa ofisi ya ZCO ilikuwa ghorofani na mara ya kukutana naye alimuuliza kama anatafutwa na Jeshi la Polisi ama hapana, ndipo ZCO alipomchukua na kumpeleka kwenye chumba kikubwa ambacho kulikuwa na Polisi nani na watu wengine takribani 30.
Alieleza kuwa akiwa mkononi amebeba begi lake la kijani alilotoka nalo safari, aliketishwa mbele ya umati huo wa watu kisha kuanza kuhojiwa, hata hivyo wakati mazungumzo yakiendelea kulikuwa na mtu aliyekaa nyuma yake akisoma gazeti ambapo kulikuwa na kitu kikimpalia.
Alieleza kuwa kutokana na hatua hiyo, alianza kupiga kelele kwamba kuna kitu kinamkera ndipo ghafla akajikuta amepoteza fahamu na hakujua nini kilichoendelea.
“Nilipopata fahamu nilijikuta nipo Hospitali ya Polisi Oysterbay ambapo wakati nikiwa kitandani nikamuona mtu aliyevalia mavazi ya Kipolisi ambaye alikuwa na nyota tatu. “Askari huyo alikuja hadi nilipolala na alitaka kunichoma sindano, lakini nilikataa na kuanza kubishana naye kwamba mimi nina daktari wangu katika Hospitali ya TMJ hivyo nipelekwe huko,” alieleza.
Alieleza kuwa wakati akiendelea kubishana na askari huyo, ghafla alijikuta anapoteza fahamu na alipozinduka alijikuta yupo Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam ambapo baadaye alipoteza tena fahamu.
Aidha, alipotakiwa kueleza kama kulikuwa na uwepo wowote wa Polisi katika Hospitali ya TMJ kati ya Machi 27 na 28, alieleza kuwa alimuuliza muuguzi wa hospitali hiyo ambapo alimwambia ofisini hapo alipelekwa na Polisi na wapo nje wanamlinda.
Pia alipotakiwa kueleza kuwa Machi 29, 2015 alipelekewa begi na washitakiwa Mnzava, Bihagaze na Milulu walimpelekea begi, alisema hakupelekewa begi na mtu, bali alikuwa nalo Polisi.
Alieleza kuwa begi lake alikuwa nalo tangu siku anakwenda Arusha kwenye kikao cha maaskofu na alikwenda nalo polisi, na ndani ya begi hilo kulikuwa na silaha, hati ya kusafiria, hundi za benki na baadhi ya nguo.
Alidai kuwa begi hilo alikuwa nalo katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), lakini baadaye muuguzi alimwambia Polisi wanalitaka begi hilo, kwani wanafanya fujo nje na walikuwa wanampiga Bihagaze ambaye ni msaidizi wake.
Hata hivyo, Gwajima alieleza kuwa aligoma kulitoa begi hilo kwa sababu lilikuwa na silaha yake, lakini baadaye akaamua kuwapatia begi hilo kwa sababu msaidizi wake alikuwa anapigwa.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Joseph Maugo alipomtaka Gwajima aeleze alifuata nini katika ofisi za ZCO wakati wito aliopewa aliitwa na aliyekuwa Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alieleza kuwa alikwenda ili kuuliza kama anatafutwa ama hapana.
Alieleza kuwa hatua ya kwenda kwa ZCO zinatokana na kuwa yeye ni Msaidizi wa Kamanda Kova, hivyo lazima angeanzia ngazi ya chini kabla ya kufika juu.
Alipoulizwa ilikuwaje washitakiwa wenzake wamo katika kesi hiyo hali ya kuwa hawakubeba begi lenye silaha, Gwajima alieleza kuwa hata yeye ameshangaa kwanini wameunganishwa.
Mbali ya Gwajima, mshitakiwa mwingine aliyejitetea ni Bihagaze ambaye alieleza kuwa Machi 29, 2015 alikuwa Hospitali ya TMJ majira ya mchana na alishinda hadi usiku.
Alidai kuwa alikuwa na waumini wengine pamoja na viongozi wa dini, ambapo kwa ujumla walikuwa zaidi ya 10. Alipoulizwa alifahamu vipi suala la kulazwa kwa Gwajima hospitalini hapo, Bihagaze alidai kuwa alifahamu kwa sababu alikuwa naye safari wakitokea Arusha hadi misukosuko ilipomkuta.
Alieleza kuwa siku ambayo Gwajiama alikwenda Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ilikuwa jioni na mara baada ya kuelekea ofisi za ZCO yeye alikwenda kununua maji na aliporudi aliambiwa Gwajima amezimia na amepelekwa Hospitali.
Alieleza kuwa akiwa katika hospitali ya TMJ majira ya jioni walifika Polisi wakiwa na silaha ambapo waliwalazimisha wakae chini, kisha wakamwambia asimame na ndipo walipoongozana naye hadi alikolazwa Gwajima wakimuaru achukue begi la kijani lilikokuwa na silaha.
Alidai kuwa aliwagomea Polisi hao lakini walimlazimisha, ndipo Gwajima alipoamua kumpa begi hilo, naye aliwapa Polisi baada ya kuingizwa kwenye gari lao.
Alisema kuwa polisi waliwachukua na kuwapeleka kituo cha Oysterbay ambako walihojiwa na kuandika taarifa zao kuhusu vitu vilivyokuwa ndani ya begi hilo.
Alidai kuwa mara baada ya kuhojiwa majira ya saa nne asubuhi walikuja askari wengine ambao walimuuliza, kwanini walitaka kumtorosha Gwajima, lakini aliwajibu kwamba hakuwa na nia hiyo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10 hadi 11, mwaka huu itaendelea kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo.
Pia katika kesi nyingine inayomkabili Gwajima ya kutumia lugha chafu na kumdhihaki Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Hakimu Mkeha aliuonya upande wa mashtaka kuhakikisha wanafika na mashahidi.
Hakimu Mkeha alisema kesi hiyo ina miaka miwili, lakini upande wa mashitaka una shahidi mmoja tu, hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 12 na 13, mwaka huu kwa ajili ya ushahidi.
Katika kesi hiyo, Askofu Gwajima kati ya Machi 16 na 25, mwaka jana maeneo ya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam alitumia lugha chafu na kumdhihaki askofu Pengo.
Inadaiwa alimdhihaki Pengo kwa kusema; “Ni mpuuzi mmoja, mjinga mmoja, asiyefaa mmoja anaitwa Askofu Pengo, aliropoka sijui amekula nini mimi naitwa Gwajima namwita mpuuzi yule, mjinga yule….”, maneno yanayoonesha kumshushia hadhi askofu Pengo kuwa mtoto mpuuzi na mwenye akili ndogo na kwamba maneno hayo yangeweza kuleta uvunjifu wa amani.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment