Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Taasisi za Serikali na Mashirika yote ya Umma kutumia kituo cha kutunzia kumbukumbu cha Taifa (National Data Centre)chenye hadhi ya juu kabisa katika viwango vya ubora na usalama wa Taarifa na Kumbukumbu. Kamati pia imezitaka Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutumia Kituo hicho katika kutunza kumbukumbu zake ili kuwa mfano kwa Taasisi nyingine za Umma.
Akizungumza katiko maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu mara baada ya ziara ya siku moja ya Kamati hiyo kuitembelea Kampuni ya Simu Tanzania TTCL pamoja na miradi ya Mkongo wa Taifa na Kituo Mahiri cha kutunzia kumbukumbu (Data Centre), Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Norman Sigala amesema, uhai wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL upo mikononi mwa Serikali ambayo ina jukumu kubwa la kuihusiha Kampuni hiyo yenye uwekezaji mkubwa.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezitaka Taasisi zote za Umma na binafsi kulipa madeni zinazodaiwa na TTCL kuiwezesha Kampuni hiyo kujiendesha kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na Watendaji wa Umma wanaogharamiwa huduma za Mawasiliano kutumia huduma za simu za TTCL katika maeneo yote yenye huduma hizo.
Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe Rita Kabati amesema, kukamilika kwa Mchakato wa kuondoka kwa Bharti Airtel ndani ya TTCL kunahitaji kwenda sambamba na uwezeshaji wa mtaji kama ilivyofanyika kwa Kampuni ya Reli Tanzania(TRL) na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambazo sasa zinafanya vizuri.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bw Waziri Kindamba amesema, ushirikiano mkubwa uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu umewezesha Serikali kuchukua hatua ambazo zimeipa TTCL nguvu mpya ya kurejea katika nafasi yake ya kihistoria ya kuwa Kinara wa utoaji huduma za Mawasiliao nchini.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na Serikali kulipa sh Bilioni 14.7 na kuhitimisha ubia usioridhisha wa Kampuni ya Bharti Airtel ndani ya TTCL uliodumu kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu bila kuleta tija iliyotarajiwa. Hatua nyingine ni pamoja na Serikali kuiruhusu TTCL kutumia majengo yake kama dhamana kuweza kupata mikopo ya Shilingi bilioni 96.6 kwa ajili ya uwekezaji, kurekebisha mizania ya Kampuni kwa kufuta madeni ya takribani Shilingi bilioni 100 hivyo kufanya Kampuni kuweza kukopesheka.
Maamuzi mengine ni Serikali kuipatia TTCL masafa ya Megahezi 1800 na 2100 ambayo yametumika kufunga mitambo ya mawasiliano ya teknolojia za 2G (GSM), 3G (UMTS) na 4G (LTE) pamoja na kuikabidhi TTCL dhamana ya kusimamia na kuendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano(NICTBB) na Kituo cha Kimataifa cha kuhifadhia kumbukumbu za kimtandao (National Internet Data Centre).
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Mheshimiwa Omari Nundu amesema, TTCL inakabiliana na changamoto kadhaa zinazohitaji utatuzi wa haraka. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na TTCL kukosa mtaji wa kutosha( Takriban shilingi bilioni 300) kunununua teknolojia za kisasa na mitambo mipya ili kuondoa miundombinu chakavu na kuongeza ufanisi na ubora wa huduma.
Changamoto nyingine ni madeni ya ankara za huduma ambayo TTCL inadai taasisi za Umma na serikali ambayo yamefikia takribani Sh Bilioni 9 ambazo endapo zingelipwa kwa wakati, zingesaidia sana kuimarisha utendaji wa TTCL.
Nao Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja Mhe Japhari Michael na Mhe Prof Anna Tibaijuka wamesema, TTCL inao wajibu mkubwa kwa Taifa kuhakikisha kuwa Mawasiliano yanafika nchi nzima na hasa katika maeneo ya Vijijini ambako Kampuni binafsi za Mawasiliano hazitoi kipaumbele katika kufikisha huduma zake.
No comments:
Post a Comment