ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 10, 2017

Lissu, wenzake wanne kupinga uchaguzi TLS

WAGOMBEA watano wa nafasi ya urais katika Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), wamekusudia kupeleka maombi ya kuunganishwa kwenye kesi ya kupinga uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Machi 18 mwaka huu, katika Mahakama Kuu.
Kesi hiyo ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo, ilifunguliwa mkoani Dodoma na mawakili wawili; Godfrey Wasonga na Onesmo Mpizile wa Dar es Salaam dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kuomba mahakama izuie uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika.
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye pia ni Mjumbe Kamati Kuu wa chama hicho, Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema jana jijini Dar es Salaam kuhusu kesi hiyo iliyofunguliwa na wanachama wenzao wa TLS kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo.
Lissu alisema katika sheria zao zilizoweka utaratibu wa kuendesha kesi mahakamani zinaruhusu mtu yeyote mwenye maslahi ya kesi husika kuunganishwa kwenye kesi hiyo kama mdaiwa ama mdai na kufafanua kuwa kama ni ya kudai anaunganishwa kama mdai na kama kutetea anaunganishwa kama mdaiwa.
“Tumepeleka maombi ya kuunganishwa kama wadaiwa ili tuweze kupinga maombi yao mahakamani. Kati ya leo na kesho tutapeleka maombi Mahakama Kuu Dodoma na Dar es Salaam ili tuunganishe kesi ile kama wadaiwa tutanunua ile kesi. “Katika muda huu tutahakikisha tunafungua maombi ili masuala ya uchaguzi huu yaamuliwe, nasi tupate nafasi ya kuzungumza,” alisema.
Alisema inapofikia masuala ya uchaguzi wa TLS kwa mujibu wa sheria na kanuni zake hayana maana kabisa kwamba mgombea hatakiwi kuwa mwanasiasa, bali ni sifa za kugombea ikiwepo kuwa wakili wa kujitegemea, mlipaji wa kodi za serikali, kuwa na leseni ya biashara na kuwa mwanachama kwa miaka 10.
Wagombea watano wanaotaka kuwania nafasi hiyo ni Lissu, Lawrance Masha, Francis Stolla, Victoria Mandali na Godwin Mwapongo.
Wiki hii Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harison Mwakyembe alisema Serikali haiwezi kuona chama hicho kinajiingiza katika siasa na wakiacha viongozi wa vyama vya kisiasa kukiongoza ni mgongano wa maslahi na Serikali haitasita kufuta sheria iliyoanzisha chama hicho.

No comments: