Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, usiku huu anahudhuria Mkutano wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaojulikana kama SADC Double Troika, mjini Mbabane Swaziland. Mkutano ambao unajadili kwa kina hali tete ya usalama katika Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo( DRC) na Nchi ya Lesotho, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Asasi hiyo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Mkutano wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaojulikana kama (SADC Double Troika) unaowahusisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika umeanza usiku huu katika ukumbi wa Grand- Lozitha mjini Mbababe Swaziland.
Katika mkutano huo, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dakta JOHN POMBE MAGUFULI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama inayojulikana kama SADC DOUBLE TROIKA kwenye mkutano huo.
Mkutano huo wa dharura utajadili kwa kina namna ya kupata suluhu kuhusu hali tete ya ulinzi na usalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)na Lesotho.
Mkutano huo wa SADC Double Troika unafanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya mkutano wa Mawaziri wa Kamati Ndogo ya Siasa na Diplomasia uliofanyika Dar es Salaam tarehe 24 februari 2017 ambapo mawaziri hao walionyesha ipo haja ya kuitisha mkutano huo ili kujadili kwa kina hali ya ulinzi na usalama kwenye hizo.
Mkutano wa SADC Double Troika unahusisha nchi Sita wanachama wa asasi hiyo ambazo ni Tanzania,Swaziland, Afrika Kusini, Angola, Botswana na Msumbiji.
Ufunguzi rasmi wa mkutano wa SADC utafanyika kesho asubuhi tarehe 19-Marchi-2017 katika ukumbi wa Grand- Lozitha mjini Mbababe Swaziland ambapo wakuu wa nchi na serikali wa SADC watajadili masuala mbalimbali ikiwemo uwezeshaji wa Chuo cha Elimu ya Sayansi na teknolojia kitakachojengwa nchini Swaziland na mkakati wa ujenzi na uendelezaji wa viwanda unaolenga kuleta mageuzi na mabadiliko katika uchumi wa viwanda kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbabane- Swaziland
No comments:
Post a Comment