ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 21, 2017

Upatikanaji wa maji Tanzania hasa katika maeneo ya vijijini bado ni changamoto

Related image
Nusu ya wananchi (Asilimia 54) ndio hupata maji kutoka kwenye vyanzo vilivyoboreshwa; asilimia 46 wakiwa wa vijijini na asilimia 74 wa mijini

Tarehe 21 mwezi wa 03, 2017, Dar es Salaam: Inaonekana kwamba hakuna mabadiliko makubwa yaliyotokea katika upatikanaji wa maji nchini Tanzania, hususani katika maeneo ya vijijini, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Ingawa kuna taarifa nyingi zenye takwimu juu ya hali ya maji nchini, ni taaarifambili tu zinashabihiana na kuonesha uwepo wa maboresho katika upatikanaji wa maji ndani ya miaka ya karibuni.
·         Utafiti wa Sauti za Wananchi umeonesha ya kwamba Upatikanaji wa maji vijijini ulikuwa asilimia 55 mwaka 2014 na asilimia 46 mwaka 2016 – Ofisi ya Taifa ya takwimu inaonyesha tofauti ya upatikanaji wa maji kuwa kati ya asilimia 40 na 50 kwa zaidi ya miaka 10 ambapo tafiti tisa kati ya kumi zimeonesha uwiano wa takwimu ndani ya kiwango hiki.

·         Wizara ya Maji  nayo imeripoti upatikanaji mkubwa wa maji wa kati ya asilimia 50 na 60 ndani ya kipindi tajwa.
·         Takwimu za Matokeo Makubwa Sasa zinaripoti kuongezeka kwa kasi ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi asilimia 67 mwaka 2015.

Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika utafiti unaoitwa Safi na Salama? Maji, usafi na Afya Mazingira. Muhtasari huu unatokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia njia ya simu. Takwimu hizi zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,808 wa Tanzania Bara mnamo mwezi Oktoba mwaka 2016 (Zanzibar haikuhusishwa katika utafiti huu).

Utafiti umeonesha kuwa, zaidi ya nusu ya wananchi (asilimia 54) wameripoti kutumia vyanzo vya maji vilivyoboreshwa katika kujipatia maji ya kunywa. Hata hivyo, kuna tofauti kubwa kati ya kaya za mijini (asilimia 74) na vijijini (asilimia 46) na kati ya makundi ya  matajiri (asilimia 75) na masikini (asilimia 41) kwenye utumiaji wa vyanzo vilivyoboreshwa.
Katika maeneo ya vijijini, vyanzo vinavyotumiwa zaidi ni visivyoboreshwa kama vile visima visivyojengewa uzio (asilimia 26) na maji ya ardhini (asilimia 20). Vyanzo hivi havijaboreshwa. Kaya chache sana zinatumia vyanzo vilivyoboreshwa kwa mfano mabomba ya umma (asilimia 17), au visima vilivyojengewa (asilimia 16).
Kwa maeneo ya mijini, vyanzo vilivyoboreshwa ni vingi. Nusu ya wakazi wa mijini hutumia maji ya bomba katika nyumba zao (asilimia 31) au kutoka kwa jirani zao (asilimia 21). Takribani mtu mmoja tu kati ya kumi wa mijini ndiyo hutumia chanzo cha maji kisichoboreshwa ikiwemo kisima kisichojengewa (asilimia 7) au magari ya kusambaza maji (asilimia 7).

Vilevile, wananchi sita kati ya kumi wameripoti kutibu maji kabla ya kuyanywa. Njia kubwa inayotumika kutibu maji ni kuchemsha (asilimia 49) ikifuatiwa na kuchuja (asilimia 27).

Pamoja na chagamoto ya upatikanaji wa maji kwa ujumla, kaya za vijijini pia zinakabiliwa na changamoto ya umbali wa kuvifikia vyanzo vya maji. Zaidi ya nusu ya wananchi (asilimia 57) hutumia zaidi ya dakika 30 ambazo ndiyo lengo la serikali kutafuta maji ikilinganishwa na asilimia 28 ya kaya za mijini. Linapokuja suala la kutafuta maji, mzigo mkubwa hubebwa na wanawake; ambapo wananchi 6 kati ya 10 (asilimia 61) wameripoti kwamba kuteka maji ni wajibu wa wanawake wasimamizi wa kaya au mke wa mkuu wa kaya. Utafiti huu pia unaonesha uwiano wa upatikanaji maji usio wa uhakika kwa mijini na vijijini. Hiyo inajidhihirisha katika usambazaji usio sawa ambapo vijijini ni asilimia 28 na mijini ni asilimia 37 tu ya wananchi wanaopata huduma za maji. Vile vile utafiti unabainisha uhaba wa vituo vya maji kwa asilimia 35 vijijini na asilimia 26 mijini.

Kwa muktadha huo, utafiti umebaini changamoto kuu tatu katika upatikanaji maji vijijini, ambazo ni umbali wa vyanzo vya maji (asilimia 39), uhaba wa vyanzo vya maji (asilimia 35) na maji machafu (asilimia 32). Kwa upande wa mijini, changamoto kubwa ni usambazaji usio na uhakika (asilimia 37), gharama kubwa za upatikanaji wa maji (asilimia 27) na uhaba wa vyanzo vya maji (asilimia 26).

Kwa upande wa uongozi na uwajibikaji, wananchi wamekiri kuwa viongozi wao wanazo taarifa za changamoto za upatikanaji wa maji. Jumla ya wananchi 7 kati ya kumi (asilimia 69) wanakumbuka kwamba mbunge wao aliwaahidi mradi wa maji katika kampeni zake za uchaguzi. Hata hivyo wananchi 3 kati ya 4 (asilimia 75) wanasema kwamba ahadi hizi hazijatekelezwa, wakati asilimia 23 wanakiri kwamba baadhi ya ahadi hizi zimetekelezwa.

Suala la kunawa mikono lilipoulizwa, wananchi 8 kati 10 (asilimia 81) waliripoti kufanya hivyo baada ya kutoka chooni, na 4 kati ya 10 (asilimia 36) walinawa kabla ya kula. Hata hivyo, wananchi wachache walisema kwamba walinawa kwa sabuni kabla ya kuandaa chakula (asilimia 10 tu), baada ya kusafisha choo (asilimia 8 tu), baada au wakati wa kumsafisha mtoto alipojisaidia (asilimia 4 tu) na kabla ya kumlisha mtoto chakula (asilimia 2 tu).

Sauti za Wananchi pia iliwauliza wananchi kama walishiriki katika shughuli za usafi kama ilivyoelekezwa na Rais tarehe 9 Disemba 2015. Karibu wananchi wote (asilimia 93) wameripoti kwamba wameshiriki,  na 7 kati ya 10 (asilimia 72) wameripoti kwamba kuna shughuli za usafi zinazoendelea katika jamii zao. Ratiba za usafi wa jamii zilizopangwa hutekelezwa zaidi katika maeneo ya mjini (asilimia 87) kuliko vijijini (asilimia 64).

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi wa Twaweza, amesema, “Suala la upatikanaji wa maji hujadiliwa mara chache sana katika vyombo vya habari. Lakini takwimu zinaonesha kwamba wananchi wengi hawapati maji safi, salama na ya uhakika. Kadiri wanavyozidi kukabiliana na changamoto hizi kila siku, wananchi wanakumbuka ahadi zilizotolewa na viongozi wa kisiasa waliofanya kampeni  za uchaguzi na kuahidi kuboresha maisha yao kwa kuwapatia maji. Inasikitisha kwamba ahadi hizi hazijatekelezwa kwa walio wengi. Hatuwezi kuipuuza sekta hii. Kuboresha upatikanaji wa maji safi, kutunza vyanzo vya maji vilivyopo, na kutilia mkazo shughuli za usafi vinahitaji ushirikiano mkubwa na mahusiano bora kati ya wananchi, serikali na watoa huduma ya maji. Wakati wa uwajibikaji ni sasa.”

Maelezo kwa Wahariri
        Muhtasari huu na takwimu zake zinapatikana kupitia www.twaweza.org, au www.twaweza.org/sauti
        Twaweza inafanya kazi ya kupima uwezo wa watoto kujifunza, wananchi kuwa na utayari wa kuleta mabadiliko na serikali kuwa wazi na sikivu zaidi katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Twaweza ina programu, wafanyakazi na ofisi katika nchi zote tatu, na utaratibu unaoheshimika kimataifa wa kujifunza, ufuatiliaji na tathmini. Programu zetu muhimu ni pamoja na Uwezo, ambayo ni tathmini kubwa ya kila mwaka ya wananchi barani Afrika inayopima viwango vya watoto vya kujifunza kwenye maelfu ya kaya, na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu ya mkononi. Pia tunashiriki kwenye masuala ya umma na sera, kupitia ubia wetu na vyombo vya habari, juhudi za kimataifa zinazoshughulikia masuala ya uongozi kama vile mpango wa Ushirikiano na Serikali wazi (OGP).
        Tovuti: www.twaweza.org Facebook: Twaweza Tanzania Twita: @Twaweza_NiSisi

No comments: